Kwao Nyerere siyo "Baba wa
Taifa" tena; kwao ni "Mzee Nyerere"; kwa watawala wetu hawa
walioshindwa wanasema wamefanya mambo mengi sana ya maendeleo kuliko
"Wakati wa Nyerere". Wanajitamba kuwa wao wamekuza sana demokrasia na
kuwa hata "Nyerere" hakuweza kufanya waliofanya wao. Katika upotofu
wao wanaamini kabisa kuwa wao wanapendwa zaidi; na wanapendwa kwa sababu
wamefanya mengi mno na hawaelewi kwanini watu hawaoneshi shukrani!
Ndio maana kila kukicha hawaachi kubembeleza
kwa wananchi kuwa "hamuoni tunayofanya" na kuwa watu wanalaumu tu
lakini hawatoi pongezi kwa "mazuri mengi". Imefika mahali Kikwete
mwenyewe amedai mahali fulani anataka kukumbukwa kuwa ni "bwana
maendeleo"; anasema hivi kwa sababu anapokaa ofisini anaamini kabisa kuwa
ameweza kuwapatia Watanzania 'vitu" vingi sana vya maendeleo kuliko wakati
wowote wa historia - vitu ambavyo hata Nyerere hakuweza kuwapatia. Kikwete
anataka awe juu ya Nyerere kwa kila kipimo kwani kipimo kilichowekwa ni
Nyerere. Na bila ya shaka kuna sababu - Nyerere hakuamini kuwa walikuwa tayari
kuwaongoza Watanzania - hawa kina Kikwete na Lowassa.
Sasa katika kumdunisha Nyerere ili wao wakue
wameacha propaganda chafu dhidi ya Nyerere na uongozi wake. Leo hii
tunashuhudia mambo ambayo - pamoja na 'ubaya' wote wa Nyerere hayakuwahi
kutokea chini ya "dhaalim Nyerere"! Matukio yanayotokea leo hii
ukiwaambia watu walioshi wakati wa Nyerere, chini ya chama kimoja na uongozi
thabiti hawawezi kuelewa yanawezekana vipi kutokea. Watu wa enzi za Mwalimu
wanakumbuka vizuri kuwa kiongozi aliyefanya madudu hakuvumuliwa; na bahati
mbaya wakati ule hatukuwa na wasomi wengi na watu wengi wenye udhoefu lakini
Nyerere hakuwaonea huruma. Wapo ambao hadi leo wana kinyongo na Nyerere kwa
sababu hakuwapa nafasi nyingine.
Lakini katika kumdharaulisha Nyerere na
kujaribu kupuuza mafanikio yake makubwa zaidi wamejikuta hawana pa kukimbilia!
Tuliokuwa wakati wa Nyerere hatukumbuki jinsi JWTZ likitumiwa kisiasa kama
linavyotumika hivi sasa! Fikiria ndege ya jeshi itumwe kumchukua raia kumpeleka
Mahakamani!? Kwamba, ati vurugu za uchaguzi zilazimishe JWTZ kuingilia kati!
Kwamba vikosi vya kutuliza ghasia vya polisi vizidiwe nguvu na mara moja
kuliingiza jeshi kufanya kazi za jeshi la polisi! Unthinkable! Lakini wao wanaamini
wako sawa!
Lakini siyo kwamba wamedharaulisha na kumtupa
nje Nyerere ni zaidi ya hivyo; wameitupa misingi ya taifa letu. Wanataka
kujenga kwa misingi ya mabua! Waliachiwa misingi ya zege lakini wao wakiamini
ni 'magenius" wameamua kutengeneza 'taifa jipya' nje ya misingi iliyounda
Tanzania. Leo hii Watanzania kwa mamilioni wananung'unika moyoni kwani
hawatambui kama hili ndilo Taifa waliloachiwa kama urithi. Sasa hivi inaonekana
Tanzania inazidi kufanana zaidi na mataifa mengine ya Afrika kiasi kwamba
linaweza lisitofautike tena mbele ya umma.
Wameitupa misingi sasa hawana cha kujengea;
wamebakia kutumainia vitisho, dharau na matumizi ya nguvu. Wameshindwa kabisa
kujenga hoja - kwa mfano kwenye hili suala la gesi. Hawana ushawishi wa hoja na
badala yake hata kauli zao wanazotoa zimejaa dharau (contempt) na matokeo yake
watu nao wanawadharau! Wanafikiri vitisho na kejeli zinajibu hoja!
Kushindwa kwa sera zao mbalimbali ni matokeo
ya kuachana na misingi ya taifa; wanafikiri wanaweza kutengeneza sera nzuri nje
ya misingi ya taifa! Matokeo yake:
Sera ya Nishati na Madini imeshindwa
Sera yao ya Gesi imeshindwa - hata kabla
haijaanza!
Sera yao ya Elimu imeshindwa
Sera yao ya siasa imeshindwa
Sera yao ya Sayansi na Teknolojia imeshindwa
Sera yao Mazingira imeshindwa
N.k
Wameshindwa lakini hawaamini wameshindwa na
badala yake wanawalaumu wanaowaambia wameshindwa kwa kushindwa kwao! Kana
kwamba, wanaowalaumu wakinyamaza basi wao wataweza! Wenyewe wanaambizana kuwa
wakipewa nafasi nyingine 2015 basi wataaanza kuweza; na wapo watu wanaamini
kuwa hilo linawezekana; kwamba pundamilia anaweza kugeuka na kuwa farasi! Kama
wenyewe wameshindwa kuvuana magembe licha ya mbwembwe zote za "kuvuana
magamba" kweli kuna uwezekanow wataweza? Na ukweli ni kuwa walipofika sasa
hawawezi kurudi kwenye misingi ya Nyerere na Taifa letu; kwa sababu kurudia
misingi hiyo ni kujishtaki katika historia.
kuna namna moja tu ya kuwasaidia... kuendelea
kuwakataa.
Maskini CCM!
Maskini Kikwete
Maskini Tanzania chini yao!
Source: Mwanakijiji
No comments:
Post a Comment