Habari wana blog:
Leo tunaendelea na mada yetu ya ujasiriamali baada ya kuwa katika mapumziko ya mwisho wa wiki, kwa kujifunza nadharia ya mambo mbalimbali yanayopatikana kwenye ujasiriamali. Chapisho la mwisho tuliona sifa mbali mbali za mjasiriamali kinadharia. Leo hii tunaenda kuangalia biashara ama miradi ambayo mjasiriamali anaweza kijishughulisha nayo ili aweze kutimiza lengo lake lake la kujipatia faida na kumridhisha mteja. Kumbuka huwezi fanya jambo lolote kwa ufasaha zaidi kama hujui nadharia ya jambo hilo kwa ufasaha zaidi.
Mradi/Miradi ni nini?
Kwa lugha ya kijasiriamali Mradi ni biashara unayoitekeleza (commercial untertaking) ima kuzalisha bidhaa ama kutoa huduma kwa lengo la la kujipatia faida na kuridhisha wateja. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya watanzania wanajishughulisha na kilimo. Kilimo hapa ni neno pana kwa maana ya uzalishaji wa mazao mfano: Mahindi, Mpunga (Mchele), viazi na mazao mengine mbali mbali unayoyafahamu, matunda, mbogamboga na maua.
Pia kilimo kinahusu ufugaji wa wanyama mbali mbali mfano: Ng'ombe, Mbuzi, Nguruwe na Kondoo:Ufugaji wa ndege Mfano: Kuku, bata, njiwa na kanga. Ufugaji huwa na lengo la uzalishaji wa bidhaa kama nyama, ngozi, maziwa, mayai na bidhaa nyingine zitokanazo na wanyama ama ndege.
Kwa hiyo mradi unaweza kuwa ni uzalishaji wa bidhaa kama tulivyoona hapo juu, pia mradi unaweza kujikita kwenye utoaji huduma. Mathalani afisa ugani ambaye ana taaluma ya utabibu wa mifugo anaweza kutibu mifugo kumi mpaka ishirini kwa siku na kulipwa ujira kwa kutoa huduma hiyo. Kuna huduma nyingi hutolewa na kisha ujira hutolewa baada ya huduma hiyo kupatikana. Mfano wa huduma hizo ni Ufundishaji (elimu), mawasiliano, ushauri, matengenezo, ufundi, usafirishaji , udalali n.k.
Somo tunaloweza kujifunza hapa ni kwamba mjasiriamali ana wigo mpana wa kuchagua aina ya mradi anaotaka kuutekeleza, aidha azlishe bidhaa ama atoe huduma. Miradi hii hutofautiana kulingana na mtaji uliowekezwa kwenye mradi husika na kufanya miradi hyo iwe ya aina mbili aidha midogo (micro enterprise) ama mikubwa (Macro enterprise).
Itaendelea: niandikie mmlanzi@yahoo.com
No comments:
Post a Comment