Na Mwinyi Sadallah | 14th August 2012
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuna haja kwa Zanzibar kurejeshewa kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN).
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa wilaya na majimbo wa Chama cha Wananchi (CUF) katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, kisiwani Pemba jana.
Alisema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti chake UN na kuelezea haja ya kuwepo kwa mamlaka kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake kwenye umoja huo.
Maalim Seif alisema hoja kubwa ambayo Wazanzibari wanatakiwa kujadili katika mchakato wa maoni ya Katiba mpya ni muundo na mfumo wa Muungano.
“Zanzibar tunayo Katiba yetu ya mwaka 1984 ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa ni la Muungano na hili haliwezi kuepukwa,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif aliwataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao kwanza katika mchakato wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba na kuacha tabia ya kutetea misimamo ya vyama badala ya maslahi ya nchi na wananchi wake.
“Katiba ya nchi ni mali ya wananchi siyo ya chama chochote, lakini najua kila chama kina katiba yake na hiyo ndiyo itabakia kuwa katiba na mwongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu zangu naomba tulifahamu hili na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza,” alisema Maalim na kupigiwa makofi na wanachama.
“Mimi najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na muungano wa mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumue…Yote hayo ni maoni na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu ukifika nendeni mkatoe maoni hayo kwa uwazi,” alisema Maalim Seif.
“Wakati wenu ukifika nendeni mkatoe maoni yenu kwa uwazi bila ya hofu hiyo ni haki yenu ya kikatiba,” aliongeza.
Alisema serikali ya Tanzania tayari imepanga ifikapo Aprili 2014,
Tanzania iwe na katiba mpya ambayo inatokana na matakwa ya wananchi wake
wa pande mbili za Muungano huo.
Ingawa Maalim Seif hakufafanua kauli yake ya Zanzibar kuwa na kiti chake katika UN, lakini anamaanisha kwamba Zanzibar inapaswa kuwa na mamlaka yake kamili.
Kwa maana hiyo ikiwa Zanzibar itarejeshewa kiti chake katika UN hapatakuwepo na Muungano tena kwa kuwa itakuwa ni nchi kamili ambayo inatambuliwa na UN na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.
Tangu Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kuanza kazi hiyo, kumeibuka
kikundi kinachofanya kampeni misikitini (Uamsho) kutaka Zanzibar
kujitenga katika Muungano huku wengine wakitetea kuwepo kwa Muungano wa
mkataba.
Vile vile, baadhi ya Wazanzibari wakiwemo mawaziri na makada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wamesema kuwa kuna haja ya kuwa na Muungano wa
mkataba kwa lengo la kumaliza kero zinazolalamikiwa.
Baadhi ya makada wa CCM waliotaka Muungano wa mkataba ni Waziri asiye na
Wizara Maalum, Mansour Yusuf Himid na mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya
Zanzibar, Ali Nassoro Moyo.
Hata hivyo, baadhi ya makada wamewashambulia na kuwatisha wanachama wa
chama hicho wanaotoa maoni tofauti na sera ya CCM ambayo ni muundo na
mfumo wa serikali mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wiki iliyopita
wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Jimbo lake la Kitope, alisema
wanaopingana na sera ya CCM kuhusu muungano warejeshe kadi zao za
uanachama badala ya kusubiri kufukuzwa.
Naye Mbunge wa Uzini (CCM), Dk. Mohammed Seif Khatib, Alhamisi iliyopita
akizungumza na waaandishi wa habari mjini Dodoma akiwa na wabunge zaidi
ya 30 kutoka Zanzibar alieleza kushangazwa na wanachama wanaotoa maoni
ya kuvunja Muungano.
Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wa CCM Zanzibar, alisema chama
hicho kinapaswa kuwachukulia hatua kwa maelezo kuwa walipata nyadhifa
zao kwa kutumia ilani ya CCM inayoeleza wazi kuwa sera yake ni ya
Muungano wa serikali mbili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment