Pages

Friday, August 3, 2012

Mheshimiwa Hawa Ghasia afungua rasmi maonesho ya kilimo kanda ya kusini


Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh Hawa Ghasia leo amefungua rasmi sherehe za maonesho ya kilimo maarufu kama nane nane akiwa kama mgeni rasmi. Kanda ya kusini inahusisha wilaya zote za mikoa miwili ya Lindi na Mtwara. Sherehe hizo zinafanyika eneo la Lindi liitwalo NgoNgo,  kilele chake ni tarehe nane mwezi huu na zitafungwa na Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamin Mkapa.

Akihutubia Wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Mh Ghasia amesema sherehe hizo ni chachu ya mabadiliko kutoka kilimo cha zamani kuelekea kilimo cha kisasa. Mh Ghasia aliendelea kusema kuwa maonesho hayo yatasaidia wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo pamoja na ufugaji.

Mheshimiwa Ghasia aliwashauri wakulima wa Lindi na Mtwara kutumia teknolojia zinazobuniwa na Taasisi ya utafiti wa kilimo ya Naliendele Mtwara, kama utafiti wa mbegu bora za kilimo ili kuongeza tija katika kazi yao ya ukulima. Aidha alisema maonesho hayo ya kanda ya kusini yanasaidia kuleta undugu na umoja miongoni mwa wananchi waishio mikoa hii ya kusini.

Katika eneo la ufugaji Mheshimiwa Ghasia aliwashauri wafugaji sasa kuingia katika ufugaji wa kisasa, ambao unamfanya amiliki wanyama wachache wenye tija, na kuepuka kuwa na wanyama wengi wanaomfanya mfugaji awe mzururaji. Katika kuepuka migongano kati ya wakulima na wafugaji alishauri kuwa ni vyema maeneo yakapimwa yajulikane kwa wafugaji na wakulima ili kudumisha mahusiano mazuri baina yao.

Pia mheshimiwa Ghasia alishauri wakulima wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kugeukia mazao mengine ya matunda, ufuta na choroko kwa kuwa yana tija na si kung'ang'ania korosho pekee. Ni vyema watakaokuwa wanajihusisha na matunda waende mbele katika kufungua viwanda viatakavyotengeneza sharubati (juice) ili kuongeza thamani ya mazao na kipato.

Mheshimiwa alimalizia kwa kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu katika zoezi la sensa na lile la kutoa maoni juu ya uundwaji wa katiba mpya ya nchi.

mkali
0688323837  

No comments:

Post a Comment