na Ratifa Baranyikwa
KUNA taarifa za kutatanisha kuhusu afya ya Spika wa Bunge, Anne Makinda,
ambapo inadaiwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Habari za ambazo gazeti hili limezipata toka nchini India kwa watu wake wa
karibu, zimeeleza kuwa Spika amelazwa tangu wiki iliyopita katika hospitali
hiyo.
Vyanzo vyetu hivyo vilisema, Spika Makinda ameongozana na watu watano ambao
wamekuwa wakionekana naye hospitalini hapo.
Hata hivyo, gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja ugonjwa unaomsumbua
kutokana na jambo hilo kuwa siri kati ya mgonjwa na madaktari wake.
Taarifa za ndani zinasema kuwa baadhi ya watu waliofika kumuona waliambiwa
kwamba anasumbuliwa na macho.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila,
alikiri kuwa Spika alikwenda nchini humo kwa shughuli mbili ikiwamo ya kufanya
uchunguzi wa afya wa kawaida.
Alisema Makinda alikwenda nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu kwenye mkutano
wa Maspika Wanawake (IPU) na baada ya kumaliza shughuli hiyo ndipo akaenda
kufanya uangalizi wa afya yake.
Kashilila ambaye hata hivyo alikwepa kuzungumzia kama Spika amelazwa,
aliishia kusema tu kwamba alipitia kufanya uangalizi wa kawaida wa afya yake na
amekuwa akifanya hivyo kila mwaka.
Kwa mujibu wa Kashilila, Spika atarejea wiki ijayo baada ya kumaliza taratibu
zote za kuangalia afya yake.
Wakati Dk. Kashilila akisema hivyo, mitandao mbalimbali ya intaneti,
ilionyesha kuwa mkutano huo wa maspika wanawake ulifanyika kati ya Oktoba 3 hadi
4 mjini New Delhi, nchini humo.
Hivyo, endapo Spika alitoka kwenye mkutano na kupitia moja kwa moja kuangalia
afya yake, atakuwa ametumia takriban siku 11 hadi kufikia leo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya intaneti, katika
mkutano huo ambao mada kubwa iliyokuwa ikijadiliwa ni masuala ya jinsia, Spika
Anne Makinda, alichangia kuhusu suala hilo akisema wanawake maspika wana jukumu
kubwa la kuhakikisha kwamba mabunge yanazingatia ujinsia.
Akichukulia mfano hatua ambazo Tanzania imechukua katika kufanikisha masuala
ya kijinsia katika Bunge, Makinda alielezea umuhimu wa maspika wanawake
kuhakikisha suala hilo linafanyika kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuanzisha
kamati ya usawa wa kijinsia pamoja na suala zima la bajeti sanjari na kuimarisha
muundo wa mabunge.
|
No comments:
Post a Comment