Pages

Saturday, October 27, 2012

Kikwete ataonya na kushangaa hadi lini?


Kwa mara nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameendelea kulalamika kuhusu rushwa ndani ya chama chake. Safari hii akifunga mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) mjini Dodoma (Oktoba 22, 2012), ameshangaa kuona eti wanawake nao wameingia katika gulio la ununuzi wa uongozi.
 
Kuendelea kulalamika kwake kunatoa tafsiri kwamba pengine yeye ni kiongozi asiyejua nguvu za kimamlaka alizonazo katika kudhibiti rushwa. Ni kama anasubiri kiongozi mwingine wa juu yake asikie anavyolalamika ili wala rushwa waogope au wajirekebishe.
 
Kwa sasa CCM, rushwa ni sikio la kufa lisilosikia dawa. Ukweli ni kwamba dawa pekee ya kukabili janga la rushwa CCM, yaani uadilifu ni kama haipo. Kama ipo basi ni adimu mno na kasi ya ugonjwa kushambua ni kubwa.
 
Malalamiko ya Kikwete kama ilivyo kwa wanachama wenzake wakiwamo wale wanaoshindwa chaguzi kutokana na kutoa kiasi kidogo cha rushwa kuliko wenzao, yamesikika sana na yanatuchosha achilia mbali kukera.
 
Baada ya kauli za mara kwa mara kutoka kwa Kikwete kuhusu rushwa CCM, tulitarajia safari hii kushuhudia vitendo vya kijasiri kukabili rushwa hiyo.
 
Kinyume chake, tunasikia ‘mashairi’ yenye vina vya kushangaa eti hata wanawake wa chama hicho nao ni wadau wa rushwa. Kimsingi, anayeshangaa wanawake hao, yeye ndiye ambaye watu wanastahili kumshangaa kwanza.
 
Watu wanapaswa kumshangaa kwa kutotambua ukweli kwamba, kufumbia macho tatizo maana yake ni kulistawisha.
 
Sisi tunamweleza Kikwete, hatushangai hali hiyo kwa sababu kila wakati yeye amekuwa kiongozi wa maneno matupu kuhusu kudhibiti rushwa ndani ya CCM.
 
Kwa sababu alishindwa tangu mwanzo na tatizo hilo kuvuka hadi kwa hao anaowashangaa, tunamshauri ajiandae kushangaa kushuhudia hata chipukizi wa chama hicho wakisaka uongozi kwa rushwa.
 
Tunamshangaa kwa kuwashangaa watoa rushwa wa kike CCM. Ajue rushwa ya sasa ni ya kimfumo si suala la mwanamke, mwanamume au mtoto. Rushwa haijifuti kwa kauli zake za kushangaa wengine.
 
Rushwa inafutwa kwa kupandikiza uadilifu na njia za kupandikiza uadilifu ni kuonya lakini inaposhindikana ni kutumia nguvu za sheria, sambamba na busara.
 
Kabla ya kuwataka wala rushwa wabadilike, Kikwete abadilike kwanza katika vita hii ngumu dhidi ya rushwa vinginevyo hali itakuwa mbaya.
 
Source: Raia mwema

No comments:

Post a Comment