Pages

Sunday, January 27, 2013

TAARIFA YA NDUGU ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA


Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara

Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.

Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.

Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.

Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara na hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.

Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro
huu.

Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.

Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.

Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.

Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.

Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili.

Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (zittokabwe.com).

Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la Mtwara.

Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.

Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.


Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara

Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.

Tufanyeje?

Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
  1. Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.
  1. Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
  1. Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.

Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa chama kutoa ridhaa.


ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Kaskazini (Chadema)
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni

Saturday, January 26, 2013

Taswira vurugu za jana Mtwara

Mahakama ya mwanzo iliyochomwa moto

                                                         Mwandishi wa Chanel 10 aliyepigwa jiwe
Kijana akishikiliwa na Askari baada ya kukamatwa

                                                     Chini ya ulinzi

                                                  Nyumbani kwa Mh. Hawa Ghasia hakukusalimika

Source: Jamii Forum

Friday, January 25, 2013

Mkuu wa kaya ilipo gesi anusurika kutekwa, wananchi wachoma moto gari

Mabaki ya gari lililochomwa
MKUU wa Kaya ya Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa mkoani Mtwara, Bibi Somoe Mtiti (106) amenusurika ‘kutekwa’ na mtu anayeaminika na wakazi wa eneo hilo kuwa ni mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa baada ya wananchi kuvamia gari lake na kuliteketeza kwa moto jana usiku.

Hivi karibuni Bibi Mtiti aliionya Serikali juu ya mpango wake wa kusafirisha gesi ghafi kwenda Dar es Salaam kwa madai iwapo itapuuza onyo hilo bomba hilo litasafirisha maji badala ya gesi iliyokusudiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa mhusika hajakwenda polisi kulalamika.

Kwa mujibu wa wanakijiji hao, mtu huyo ambaye ana asili ya kijiji hicho waliyemtambua (jina linahifadhiwa) aliwasili kijijini hapo jana saa 10 jioni akiwa na gari dogo aina ya Mark II na kwenda nyumbani kwa shangazi yake.

Habari zinadai kuwa saa 2 usiku mshukiwa huyo alidaiwa kwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti akiwa na gari pamoja na shangazi yake.“Unajua yule bibi tunamlinda, sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu wakaanza kujiuliza linafanya nini…wakaanza kusogea, kadiri muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo watu walivyozidi kuongezeka,”alisema Juma Ayoub mkazi wa kijiji hicho.

Asha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi Mtiti, akihadithia juu ya tukio hilo, alisema yapata saa 2 usiku wakiwa wanakula chakula walipokea wageni wawili ambao baada ya kumaliza kula waliomba kuongea na mkuu huyo wa kaya.

“Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na bibi…alimuuliza bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu hawezi…wakaniuliza mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia siwezi…akasema ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia...wamjie bibi wakazungumze naye mambo ya gesi,” alisema Hamis.

Aliongeza kuwa “Kama bibi yupo tayari Jumanne ijayo watamfuata kwa gari…mimi nikasema sitaki…nilipochungulia nje nikaona watu wengi wamezunguka.”

Kwa upande wa mtoto mwingine wa bibi huyo alisema,” Kwa kuwa tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia haufai, akawa anabisha, tukaendelea kumsihi..wakati huo watu wanazidi kuongezeka…alipotoka akakosea njia, alipopita hakukuwa na njia…watu walimfuata wakaanza kumrushia mawe…aliacha gari akakimbia…ndipo wananchi walipoliteketeza gari kwa moto,” alisema Manzi Mohamedi Faki mtoto wa tano wa Bibi Mtiti.

Shangazi wa mtuhumiwa amethibitisha kumpokea mwanaye huyo na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimwomba mkuu huyo wa kaya akubali kuondoka naye kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ametumwa na viongozi wake wa juu.

“Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu pale, naye alikimbia na ndipo walipochoma moto gari,” alisema shangazi huyo.Alifafanua kuwa “Huyu mwanangu anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi Usalama wa Taifa…nadhani alirudi jana hiyohiyo Mtwara.”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Tostao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ofisi yake haikupokea mgeni yeyote kutoka serikalini kwa siku hiyo. “Ni kweli gari limechomwa lenye namba za usajili T 609 BXG mali ya Mussa Babu…taarifa hii ni kwa mujibu wa nyaraka tulizookota kutoka ndani ya gari hilo,” alisema Tostao.
 
Selemani Babu alikanusha madai ya yeye kwenda kijijini hapo jana na alisema, “Hapana, hapana labda umekosea…na..na..na..umekosea…sijakwenda Msimbati jana…kwa nini asiwe Mussa, umekosea siyo mimi kwa heri.”
 
Source: Mwananchi

Thursday, January 24, 2013

Moto wa gesi wavuka nje ya mipaka

 
BALOZI wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik ameonya kuhusu hatari za kugeuza suala la gesi ya Mtwara kuwa mtaji wa kisiasa.

Wakati Norway ikisema hayo, Mkurugenzi wa Uchumi katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Nyamajeje Weggoro amesema mgogoro huo utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano yaliyojaa lugha na kauli laini isiyo na vitisho wala kuwabeza wananchi.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na mijadala, mizozo na maoni kutoka kwa kada mbalimbali kuhusiana na suala la gesi hiyo inayopatikana katika eneo la Msimbati, Mtwara.

Akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa, Lushoto mkoani Tanga, Balozi Klepsvik alisisitiza kuhusu haja ya Watanzania kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya kuangalia masilahi ya watu binafsi au taasisi.

“Norway ilipogundua nishati ya petroli tulikubaliana kitu kimoja kwamba suala hili lisihusishwe na kampeni za kisiasa. Hii itasaidia kuweka mbali masuala ya rasilimali na siasa,” alisema.

Balozi huyo alisema gesi ya Mtwara inapaswa kuwanufaisha wananchi wa Mtwara kwanza kabla ya watu wengine, lakini masilahi ya taifa lazima yawekwe mbele katika mjadala wa suala hilo.

Klepsvik alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika masuala muhimu ya maendeleo na kueleza kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kwa kuwahusisha watu wa kada zote hasa wanawake.

Hata hivyo, alisema endapo mambo yatafanyika kwa utaratibu wake, gesi iliyovumbuliwa inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yao.

“Tulipogundua gesi na petroli, hatukuwa tunafahamu lolote, tuliita wageni wakatufanyia kazi ya kuchimba, wakati huo tulipeleka watu wetu vyuo vya nje kusoma na baada ya miaka 10 sasa tunashughulika wenyewe na kila kitu kwa manufaa ya taifa zima,” alisema Klepsvik.

EAC yashauri mazungumzo
Akizungumzia mgogoro huo, Dk Weggoro alisema umetokana na wananchi kutopata elimu ya kutosha kuhusu namna watakavyofaidika na rasilimali hiyo inayopatikana katika eneo lao.

“Mgogoro wa gesi Mtwara utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano lakini siyo vitisho,” alisema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya EAC jana.

Alisema haamini kama ni kweli wananchi wa Mtwara hawataki Watanzania wenzao wafaidike na gesi inayopatikana mkoani humo, bali wanahofia hatima ya maisha, faida na masilahi yao kutokana na rasilimali hiyo.

“Viongozi lazima wazungumze, wajadiliane na kufikia mwafaka na wananchi (wanaMtwara), kuhusu mambo yanayogusa maisha na masilahi yao. Ni vyema watu ambao maliasili na rasilimali zinapatikana katika maeneo yao wanufaike kwanza kabla ya wengine.”
 
Soma zaidi.....Mwananchi

Tuesday, January 22, 2013

Vigogo Bandari wafukuzwa kazi

Waziri wa uchukuzi Dr Harison Mwakyembe amewatimua kazi vigogo watano wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA), baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka , ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Soma zaidi....Habari leo

Wednesday, January 16, 2013

Mbatia: Umbea umechochea yaliyomkuta


 
MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema yaliyomkuta kwenye yake ziara mkoani Mtwara ambako amelazimika kuikatisha, yametokana na umbea aliouita ni wa mwaka 2013.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, alisema hayo jana kwenye Ofisi za Bunge Dar es Salaam.

“Unasemaje (anamuuliza mwandishi), ngoja nikwambie kilichotokea kimetokana na umbea tu wa mwaka mpya 2013, wewe tambua hivyo na sitazungumza lingine zaidi,” alijibu kwa kifupi akionyesha kukwepa kulizungumzia suala hilo zaidi.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini viliripoti kuhusu Mbatia akiwa na wabunge wa chama chake, Moses Machali (Kasulu Mjini ) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) walilazimika kujifungia ndani ya ofisi za NCCR- Mageuzi wilayani Mtwara Mjini.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya baadhi ya wananchi kuamua kumrushia chupa tupu za maji, huku wakimfuata kabla ya kuizingira ofisi hiyo wakiimba nyimbo za kumshtumu kuwa ni mamluki.

Ilielezwa kuwa, hali ilikuwa tete eneo la ofisi hiyo hasa baada ya giza kuingia, kwani wananchi walianza kurusha mawe juu ya ofisi hiyo na wengine kujaribu kuvunja mlango na kurusha vitu vinavyodiwa kuwa ni baruti zinazotumika kuvulia samaki .

Hali hiyo ilisababisha polisi waliofika kumuokoa kutumia mabomu ya machozi.
Mapema mwaka huu baadhi ya wananchi wa Mtwara waliandamana wakipinga gesi kusafirishwa kuletwa Dar es Salaam.
Badala yake, walitaka mtambo wa kuzalisha umeme kujengwa mkoani humo.

Source: Mwananchi

Tuesday, January 15, 2013

Unyama mkubwa Mbeya, wawili wazikwa hai

WAKAZI wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Watu hao, Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, walizikwa wakiwa hai pamoja na aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, marehemu Nongwa Hussein.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa tano na sita mchana, muda mfupi kabla ya maziko ya Hussein.

Kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu, Molela na Nachela kwa nyakati tofauti walipigwa hadi kuzirai na watu wanaodaiwa kushiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hussein.

Silwimba alisema Hussein alifariki dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini inaonekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa huo ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jana mchana, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Momba aliyefahamika kwa jina la Wendo aliongoza operesheni ya kufukua kaburi walimozikwa watu hao, ambao walikutwa wakiwa wameshafariki dunia.

Silwimba alisema miili ya Molela na Nachela ilifanyiwa uchunguzi, kisha kukabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao ambao waliifanyia mazishi jana mchana.

Mkasa wenyewe
Kundi la vijana tisa ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakichimba kaburi la marehemu Hussein walianza msako katika Kijiji cha Karungu wakiwatafuta wale waliowatuhumu kwamba ni wachawi na kwamba walihusika na kifo chake.

Silwimba alisema katika harakati zao, walikwenda nyumbani kwa George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu lakini hawakumkuta, hivyo kuamua kuchoma moto nyumba yake kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho.

“Baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda hadi nyumbani kwa Mzee Molela kisha wakamkamata na kumpiga sana hadi hali yake ikawa mbaya kisha wakambeba hadi eneo la maziko,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea kwenye msiba walimkuta Mama Nachela naye wakamkamata na kuanza kumpiga hadi akazimia na yeye pamoja na Molela waliwavuta hadi kwenye kaburi ambako mazishi ya Nongwa (Hussein) yalifanyika.”

Alisema baada ya jeneza kushushwa kaburini, vijana hao wanaodaiwa kwamba walikuwa na hasira walimvuta Molela na kumwamuru kuweka udongo kaburini, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya kushindwa walimsukumiza kaburini na baadaye walimvuta yule mama (Nachela) ambaye naye alikuwa hajitambui na kumtupa ndani ya kaburi halafu wakawafukia wote, kisha wakaondoka,” alisema Kaimu Ofisa Mtendaji huyo.
 
Alisema mwingine aliyekuwa akisakwa na vijana hao ni Fotino Sichilongwa na kwamba kabla ya kufanya vitendo hivyo, vijana hao walimkamata Mwenyekiti wa Kitongoji, Alfred Kukwe na kumfunga miguu na mikono kwa kutumia kamba, wakamlaza kifudifudi, kisha kumnyang’anya simu yake ya kiganjani ili asiweze kutoa taarifa kokote.
Alisema Kukwe alifunguliwa kamba hizo saa saba na nusu mchana na ndipo alipopiga simu sehemu mbalimbali kutoa taarifa za tukio hilo.

Silwimba alisema baada ya taarifa hizo kusambaa kijijini Karungu, mwenyekiti wa kijiji hicho na ofisa mtendaji wake, walikimbia na kwenda kujificha kusikojulikana wakihofia kudhuriwa na vijana hao.

“Polisi walipofika jana (juzi) jioni walikuta vijana wote waliohusika wamekimbia na hawajulikani walipo maana nyumba zao zimefungwa, hili ni tatizo kubwa maana limesababisha taharuki kubwa hapa kijijini,” alisema.

Wawili mbaroni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kulikuwa na taarifa kuwa Molela na Nachela wana undugu. Hata hivyo, habari kutoka kijijini Karungu zimesema hawana undugu wowote.

Kamanda Diwani ambaye aliwashutumu wananchi kwa kujichukulia sheria mkononi, alisema hadi sasa watu wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.“Tunawashikilia watu wawili ambao tunaamini walikuwa vinara wa tukio hili la mauaji,” alisema Diwani.
Kamanda huyo aliitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake waheshimu na kutii sheria bila shuruti na kuachana na imani za kishirikina.

“Kila mmoja afanye mambo yake kwa kujiamini. Hii ya kuendekeza imani za kishirikina ina madhara na zaidi ni kurudisha nyuma maendeleo. Jamii inatakiwa kutafuta njia halali kufikisha kero na malalamiko badala ya kutumia vurugu na fujo na kusababisha mauaji.”
 
Source: Mwananchi

Saturday, January 12, 2013

JK alaumiwa Marekani mauaji ya Mwangosi, kutekwa kwa Ulimboka


Kuuawa kikatili kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi na tukio la kutekwa, kuteswa kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, limechukua sura mpya ambapo sasa limetinga katika Seneti ya Marekani, Tanzania Daima Jumamosi limeelezwa.

Taarifa kutoka Washington nchini Marekani zinasema Rais Jakaya Kikwete amelalamikiwa rasmi katika Seneti na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu nchini, na kwamba masuala hayo sasa yatafikishwa kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binadamu (UNHRC) kwa hatua zaidi.

Mbali na mauaji ya Mwangosi na tukio la Dk. Ulimboka, Rais Kikwete pia amelalamikiwa kwa kufumbia macho matukio mengi ya kuteswa na kuuawa kwa raia pamoja na kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la uchunguzi la MwanaHalisi, kutoroshwa wanyama hai kwa kupelekwa nje ya nchi na hatua ya polisi kutumia silaha za kivita kupambana na raia wasio na silaha wakiwemo wanafunzi wanaoandamana.

Ripoti hiyo ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu yenye kurasa 27, inatuhumu utawala wa Rais Kikwete kwa kukandamiza demokrasia kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya dola.

Watetezi hao wa haki za binadamu, wamedai kuwa baada ya kufanikiwa kuingiza masuala haya ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika Seneti ya Marekani, sasa wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha suala hili linafikishwa Umoja wa Mataifa kwa kile walichokiita, kuiadabisha serikali.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana, na pia kusambazwa katika baadhi ya taasisi za habari, suala hilo liko mikononi mwa Seneta Kerry, ambaye baada ya majadiliano katika Seneti, ripoti hiyo itapelekwa UNHRC.

Habari zinasema baadhi ya wajumbe wa Seneti waliofanikiwa kuona ripoti hiyo wamemeshitushwa na kile walichokishuhudia katika picha zilizoambatanishwa.

Aidha, ripoti hiyo pia imeeleza jinsi rushwa ilivyoshamiri nchini, ukandamizaji juu ya uhuru wa maoni na matumizi mabaya ya vyombo vya dola kudhibiti vyama vya upinzani na kutumia silaha za kivita kupambana na raia wasio na silaha.

Ripoti hiyo ya kuishitaki Serikali ya Kikwete, pia imelaani vitendo vya polisi kusambaratisha maandamano ya wanafunzi wa shule za msingi jijini Dar es Salaam, walioandamana Julai 31, mwaka jana kupinga ukosefu wa walimu nchini.

Mgomo wa wanafunzi ulikuja baada ya walimu wa shule za msingi na sekondari kupitia jumuiya yao - Chama cha Walimu Tanzania (CWT) – kuitisha mgomo nchi nzima wa kutaka kuboreshwa kwa mazingira ya kazi zao, nyongeza ya mishahara na malimbikizo ya posho.

Nyaraka zilizowasilishwa na wanaharakati hao, zimeambatanishwa na picha zinazoonesha namna Jeshi la Polisi lilivyohusika kuuawa kwa Mwangosi, picha mbaya ya maiti ya mwanahabari huyo, na namna Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alivyokuwa akishuhudia askari wake wakimsulubu mwanahabari huyo kabla ya kufunga kazi kwa kumaliza uhai wake.

Kadhalika, kumeambatanishwa picha zinazoonesha maiti za watu waliouawa wakati wa maandamano huko Arusha, na ile inayosadikiwa kutokea kule Songea. Picha nyingine za kusikitisha ni zile zinazoonesha askari zaidi ya watano wakimdhibiti mwanaharakati mmoja katika maandamano, na umati wa wanafunzi wa shule za msingi wakiandamana, huku nyingine zikionesha askari mwenye silaha ya kivita akimsindikiza mwanafunzi wa kike mwenye mfuko wa madaftari.

Tangu mwaka 2005 ambapo masuala mazito ya rushwa yamekuwa yakiibuliwa, ikiwamo ununuzi wa rada feki, wizi wa fedha za umma kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mkataba tata wa Richmond, ukusanyaji wa kodi, utoroshwaji wa wanyama hai, wizi wa nyara za serikali, ikiwamo pembe za ndovu, baadhi ya wananchi wamekuwa wakituhumu serikali kushindwa kuchukua hatua.

Vilevile, wananchi wamekuwa wakituhumu Serikali ya Kikwete, kukumbatia wezi wa fedha za umma katika halmashauri za miji na wilaya, uporaji wa ardhi unaofanywa na makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi.

Jana, Tanzania Daima Jumamosi haikufanikiwa kumpata Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu kuzungumzia iwapo serikali ina taarifa juu ya jambo hili kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita muda wote bila kupokelewa.


Kova ajivua
Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova jana ametangaza rasmi kujivua katika sakata zima la kuchunguza kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.

Aidha, Kova pia amekanusha madai ya kuunda tume kuchunguza suala hilo, akitaka asiulizwe jambo lolote, huku akisukuma tukio hilo kwa wakubwa wake.

Juzi, Kamanda Kova aliliambia Tanzania Daima kwamba, jana angeweka wazi suala hilo ili Watanzania wajue kilichojiri kuhusiana na kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, jambo ambalo limetikisa anga, likiwemo lile la kukamatwa kwa raia wa Kenya, Mulundi anayedaiwa kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, jana Kamanda Kova aliruka kimanga na kudai kwamba wenye uwezo wa kulitolea maelezo ni wakuu wake wa kazi, kwa maana ya Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

Kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza utekaji huo, Kova alisema kilichofanyika wakati huo ni kuundwa kwa jopo la uchunguzi ambalo taarifa zake hazina ulazima wa kutolewa mbele ya jamii zaidi ya kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa kile walichokibaini.

Alisema baada ya kukamilisha kazi yake, alipeleka jukumu la kupeleleza sakata hilo katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini (DCI) ambayo ndiyo yenye jukumu la kutoa maelezo
Source: Tanzania daima

Thursday, January 10, 2013

Mtuhumiwa wa Ulimboka apigwa, afichwa

 
SAKATA la mtuhumiwa, Joshua Mulundi, anayekabiliwa na kesi ya kumteka na kutaka kumsababishia kifo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, sasa limechukua sura mpya baada ya kudaiwa kuondolewa kiaina katika mahabusu ya Gereza la Keko na kufichwa katika selo ya adhabu.

Chanzo chetu ndani ya mahabusu hiyo kilieleza kuwa mshitakiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya, alikuwa ameanza mgomo wa kutokula, kisha kupanda juu ya paa la gereza hilo, akitishia kujiua endapo wapelelezi wa kesi yake hawatafanya juhudi za kumleta Dk. Ulimboka ili amtambue.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mulundi baada ya kukaa juu ya paa na kunyeshewa mvua kwa saa kadhaa akiwa na mahabusu wenzake, uongozi wa gereza ulitumia nguvu za ziada kuwashusha watuhumiwa hao kwa nguvu huku mtuhumiwa huyo akipatiwa kipigo kikali kabla ya kuhamishwa.

Kwamba, Magereza waliwaleta baadhi ya askari wake wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Fujo, ambao inasemekana walimcharaza Mulundi na wenzake na kisha kumwondoa ndani ya mahabusi hiyo na kupelekwa sehemu isiyojulikana.

Tanzania Daima ilifanya juhudi za kuzungumza na msemaji wa Magereza, Omary Mtiga, lakini hakuwa na ushirikiano wa kutosha, badala yake alitoa maneno ya kejeli kwa gazeti hili kuwa linaandika habari za kizushi.

“Mimi ndiye msemaji wa Magereza, huo umbea unaopenyezewa na hao wanaojiita vyanzo vya ndani, si ‘official’ (rasmi). Mulundi anachotaka ni kuonana na hakimu kwa tarehe aliyopangiwa,” alisema.

Mtiga bila hakukubali wala kukataa, alipoulizwa uongozi wa gereza hilo umemsaidiaje kufikia anachokitaka kama mahabusu mwenye haki zake, alijibu kwa hasira kuwa hayo ni mambo ya ndani ya utawala.

“Wewe kama unataka kufanya uchunguzi wa kina wa jambo hili unalolihangaikia, njoo ufungwe gerezani, utapata yote. Hayo unayoniuliza ili niseme amepelekwa wapi ni mambo ya ndani, hayawahusu kuandika,” alisema.

Mtiga ambaye alikuwa akizungumza kwa mkato kwenye simu yake ya kiganjani, alihoji kama mwandishi anaweza kuandika masuala ya mgogoro wa ndoa yake hadharani na kusisitiza kuwa; ‘Hayo mambo ya kutafuta habari za hovyo hovyo yaacheni.”

Alisema kuwa anashangazwa kuona Tanzania Daima lilivyolivalia njuga sakata hilo wakati mshitakiwa Mulundi ni mahabusu kama wengine, asiye na sifa yoyote ya pekee.

Mtiga licha ya kusisitiza kuwa mahabusu huyo hajagoma kula, bado hakuweza kuthibitisha amehamishiwa gereza gani, akisema hiyo ni siri ya utawala.

Gazeti dada na hili la Tanzania Daima Jumapili iliyopita lililitoboa siri jinsi Mulundi anavyoitaka serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili afanyiwe gwaride la utambulisho kubaini kama alihusika katika tukio la kumteka.

Imeelezwa kuwa amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa kesi ambayo tangu Julai 3, mwaka jana bado iko kwenye hatua ya upelelezi na hajui utakamilika lini.

Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kutoka ndani ya gereza hilo alikiri kuwa mtuhumiwa huyo amegoma na usiku wa kuamkia juzi alishinda juu ya paa la gereza hilo akinyeshewa mvua.

Habari zaidi zinasema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambaye hana wakili mahakamani, wamewasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria.

Kwa mujibu wa ndugu hao, hadi sasa hawaoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika mahakamani upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.

Hata hivyo Mulundi anadai kuwa amewahi kutoa malalamiko kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa kesi hiyo unafikia tamati.

Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa nchini kwa wakati tofauti mwaka jana; alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalamu kutoka ndani ya jeshi hilo iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi ya watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi sasa Mulundi ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.

Hata hivyo tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajahojiwa, huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.

Hivi karibuni jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, limekanusha kuwapo kwa tume hiyo, likisema walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za polisi.

Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye hivi karibuni alikiri kuwapo kwa tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya kukamilisha wajibu wake.

Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk. Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.

Chanzo: Tanzania Daima

Friday, January 4, 2013

Zitto aivua nguo serikali maandamano ya Gesi Mtwara

 
Na Zitto Kabwe
'Dar inachangia asilimia 80 ya mapato. Kitovu cha Uchumi. Dar inachangia 90% ya ufisadi. Uti wa mgongo wa ufisadi nchini'
Malumbano kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri wa nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni dalili ya Serikali kuweweseka.

Katika kauli ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari, Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yetu.

Moja, Serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa kupitia zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector study 2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010). Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu. Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni -(sawa ni shilingi trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50 nyuma kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao la Korosho miaka nenda miaka rudi?

Pili, Serikali imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel, Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa ‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika kulinda uhuru wa Taifa letu?

Tatu, Serikali inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio inazalisha asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni aibu Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi Ofisi zao Kuu zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi.

Hata hivyo inawezekana kuwa ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya mapato ya nchi. Basi na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya ufisadi wote nchini. Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es Salaam na fedha nyingi za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.Mwisho, maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi. Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo. Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani 76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega.

Kampuni ya Resolute ya Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14, -Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3 bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola 11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?

Pia watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?

Uwajibikaji katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.
 
Source: Jamii Forum

Papi Kocha amuangukia JK


 
MF/NA: 836'04|Johnson Nguza (Papii Kocha)
Gereza Kuu Ukonga
S.L.P 9091
Dar es Salaam
                         
                                Mh. Rais wa Jamuhuri ya MuunganoTanzania
 
YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.

Husika na somo hilo hapo juu. Mimi ni mfungwa katika gereza kuu la Ukonga. Kwa heshima na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya ki MUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliyokabidhiwa na jamuhuri ya muungano wa Tanzania, naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais.

Na kuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais Kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu. Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais.

Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi. Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu.

Mungu akubariki Wako mtiifu
NO:836'04 JOHNSON NGUZA
(PAPII KOCHA)

Angalia barua iliyoandikwa kwa mkono hapa: http://ladyjaydee.blogspot.com/2010/02/nimetumiwa-barua-na-papii-kocha-toka.html