Pages

Wednesday, July 31, 2013

Mambo ya kuangalia katika kuanzisha Mradi


Habari wanablog:

Hakika kwa yeyote anayetaka kuanzisha biashara yampasa kuwa makini na aina ya biashara anayotaka kuanzisha. Kumbuka lengo la kuanzisha biashara (mradi) ni kujipatia faida ama kuhakikisha mteja anaridhika na kile anachokipata. Kuna mambo ya msingi kadhaa ambayo mjasiriamali anaweza kutumia kama muongozo katika kuanzisha mradi mpya.

Uainishaji wa Fursa (opportunity identification)

Kabla hujaanzisha mradi jambo la muhimu na la msingi ni kuainisha fursa zilizopo katika eneo linalokuzunguka. Fursa ni mazingira chanya na saidizi ambayo mjasiriamali anatumia kuanzisha mradi na kujipatia faida nyingi kwa muda mfupi ama mrefu. Mara tu mjasiriamali anapotambua fursa zilizopo na kuamua kuanzisha mradi, akijua kuwa matarajio ya mradi huo ni chanya basi mjasiriamali huyo uwekezaji wake una matarajio yafuatayo.
  • Mradi kuwa na mapato mazuri na endelevu
  • Mradi kuwa na soko la uhakika
  • Gharama za uendeshaji wa mradi kuwa nafuu
  • Mradi kuwa na uwezekano wa kukua.
Utakapojiridhisha kuwa hayo ya juu yanaweza kudhihiri, basi unaweza kuwekeza na kuanzisha mradi wa bidhaa ama utoaji huduma, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa upatikanaji wa faida.
 
Vyanzo vya utambuzi wa fursa
 
  • Mabadiliko ya teknolojia- hapa tumeona jinsi makundi mbalimbali yalivyofaidika na mabadilikoya teknolojia..Mfano watu wamejiajiri kupitia huduma za simu na kujipatia faida kupitia M-pesa, Tigo-pesa, Airtel money.....zamani fursa hizi hazikuepo. Pia kuna blogs za kibiashara mbali mbali zimeanzishwa nia na lengo ni kujipatia kipato kupitia kwa wadhamini: Mfano Mjengwa blog, Michuzi blog na jamii forum. Bado hujachelewa fursa zinazopatikana juu ya mabadiliko ya teknolojia zipo nyingi na kwenye sekta tofauti tofauti.
 
  • Uelewa- Kwenye jamii yoyote uelewa wa mambo unapoongezeka huambatana na fursa mbali mbali za kiuchumi zinazoendana na kuongezeka kwa uelewa. Mathani mahitaji ya vyakula vilivyo salama na kemikali umekuwa mkubwa, kulinganisha na vyakula vinavyotokana na kemikali, hii ina sababishwa na watu kuwa na elimu juu ya madhara ya kemikali mwilini.
 
  • Mabadiliko ya sera-
Itaendelea: Niandikie mmlanzi@yahoo.com
 

Monday, July 29, 2013

Mradi ama biashara (Enterprise)


Habari wana blog:

Leo tunaendelea na mada yetu ya ujasiriamali baada ya kuwa katika mapumziko ya mwisho wa wiki, kwa kujifunza nadharia ya mambo mbalimbali yanayopatikana kwenye ujasiriamali. Chapisho la mwisho tuliona sifa mbali mbali za mjasiriamali kinadharia. Leo hii tunaenda kuangalia biashara ama miradi ambayo mjasiriamali anaweza kijishughulisha nayo ili aweze kutimiza lengo lake lake la kujipatia faida na kumridhisha mteja. Kumbuka huwezi fanya jambo lolote kwa ufasaha zaidi kama hujui nadharia ya jambo hilo kwa ufasaha zaidi.
 
Mradi/Miradi ni nini?
Kwa lugha ya kijasiriamali Mradi ni biashara unayoitekeleza (commercial untertaking) ima kuzalisha bidhaa ama kutoa huduma kwa lengo la la kujipatia faida na kuridhisha wateja. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya watanzania wanajishughulisha na kilimo. Kilimo hapa ni neno pana kwa maana ya uzalishaji wa mazao mfano: Mahindi, Mpunga (Mchele), viazi na mazao mengine mbali mbali unayoyafahamu, matunda, mbogamboga na maua.
 
Pia kilimo kinahusu ufugaji wa wanyama mbali mbali mfano: Ng'ombe, Mbuzi, Nguruwe na Kondoo:Ufugaji wa ndege Mfano: Kuku, bata, njiwa na kanga. Ufugaji huwa na lengo la uzalishaji wa bidhaa kama nyama, ngozi, maziwa, mayai na bidhaa nyingine zitokanazo na wanyama ama ndege.
 
Kwa hiyo mradi unaweza kuwa ni uzalishaji wa bidhaa kama tulivyoona hapo juu, pia mradi unaweza kujikita kwenye utoaji huduma. Mathalani afisa ugani ambaye ana taaluma ya utabibu wa mifugo anaweza kutibu mifugo kumi mpaka ishirini kwa siku na kulipwa ujira kwa kutoa huduma hiyo. Kuna huduma nyingi hutolewa na kisha ujira hutolewa baada ya huduma hiyo kupatikana. Mfano wa huduma hizo ni Ufundishaji (elimu), mawasiliano, ushauri, matengenezo, ufundi, usafirishaji , udalali n.k.
 
Somo tunaloweza kujifunza hapa ni kwamba mjasiriamali ana wigo mpana wa kuchagua aina ya mradi anaotaka kuutekeleza, aidha azlishe bidhaa ama atoe huduma. Miradi hii hutofautiana kulingana na mtaji uliowekezwa kwenye mradi husika na kufanya miradi hyo iwe ya aina mbili aidha midogo (micro enterprise) ama mikubwa (Macro enterprise).
 
 
Itaendelea: niandikie mmlanzi@yahoo.com
 
 

Friday, July 26, 2013

Mjasiriamali na Mfanyabiashara


Habari wana blog:

Chapisho la mwisho tuliona kwa ufupi na maana nyepesi ya neno ujasiriamali na kuangalia jinsi mjasiriamali anavyowezesha kutumia rasilimali ardhi, watu, maji na mtaji kuweza kufanya uzalishaji aidha wa mazao (bidhaa) ama kutoa huduma kwa lengo la kujipatia faida.
 
Ubunifu
Bado neno Mjasiriamali linaweza kuwa na maana nyingi ikiwemo ya uwezo wa mtu (mfanyabiashara) kubuni (innovations) kitu (vitu) vipya na kuvitambulisha katika jamii inayomzunguka katika jitihada ya kufanya vitu hivyo viwe na uwezo wa kujikwamua kiuchumi.
 
Kumbuka sio wafanyabiashara wote ni wajasiriamali, ila wajasiriamali wote ni wafanyabishara. Sifa mojawapo ya mjasiriamali ni kuwa mbunifu wa vitu vipya (bidhaa ama huduma). Huduma kama njia mojawapo ya kupata faida ni kama vile haifahamiki miongoni mwa watanzania wengi. Wengi wetu hufikiri ili uweze kupata kipato ni vyema ukauza bidhaa, huku utoaji wa huduma ukiachwa kwa watu wachache ambao hutumia fursa hiyo kupata faida kubwa.
 
Hivyo ubunifu huweza kusababisha biashara mpya kujitokeza na kuajiri ama kutumika kama ajira binafsi kwa msururu wa wafanyabishara wengine (duplication). Hapo juu tumeona kuwa si wafanyabiashara wote ni wajasiriamali, ila wajasirimali wote ni wafanyabiashara. Hii ni kwa sababu mjasiriamali ana sifa za ziada na za kipekee kumshinda mfanyabiashara.

Sifa hizi za ziada za mjasiriamali ni Mbunifu (innovator), kujitegemea (independent), kujiamini (self-confidence), mpangiliaji (organized), muono (vision), sugu (persistent), Tumaini (optimism), commited, mtendaji (action-oriented), mtatuzi wa matatizo (problem solver), kujihusisha na hatari: kutoogopa kupata hasara (risk taker) na anayenyumbulika (flexiblity).

Sifa hizi ni za mjasiriamali aliyekamilika na aghalabu kukuta mfanyabiashara kuwa nazo. Usihofu kama hauna kipaji cha ubunifu, unaweza kuiga mambo mazuri kutoka kwa wabunifu na ukayatumia ili uweze kujikwamua kuchumi.
 
Itaendelea
 
 Unaweza kukomenti kwenye hii blog :

 Ama niandikie maboresho kwenye mmlanzi@yahoo.com
 

Thursday, July 25, 2013

Ujasiriamali ni nini?

Wapenzi wa blog hii nimeamua kubadili mfumo wa blog hii kutoka katika kuleta taarifa mbali mbali za kijamii na kujikita zaidi na dhana nzima ya ujasirimali. Blog hii itakuwa inakuletea tips mbalimbali za ujasiriamali kwa kadiri ya uwezo utakavyokuwa unapatikana. Hivyo nategemea mafunzo mengi pia kutoka kwa wasomaji wa blog hii ili tuweze kuondoka katika mzunguko huu wa umasikini.
 
 Lengo kuu ni kusaidia watanzania wenzangu kujua mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wafanyabiashara mbali mbali kupata mafanikio ya kibiashara, kutumia mbinu hizo kwa kuiga ama kuibua mbinu mbadala ili tuweze kuondokana na umaskini.
 
Huku idadi ya watu ikizidi kuongezeka duniani na Nchini kwetu kwa ujumla, changamoto kuu imekua suala la ajira. Kila mmoja wetu anataka kuajiriwa aidha serikalini ama kwenye sekta binafsi huku suala la kujiajiri likiwa la mwisho katika vipaumbele.
 
Ujasiriamali ni nini?
 
Kwa sasa ni jina maarufu sana hapa Tanzania, mtu yeyote aliyefanikiwa katika biashara hupewa jina hili. Maana ya ujasirimali inabaki katika uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wa kutumia rasilimali chache zinazokuzunguka vizuri ili uweze kupata faida.
 
Mathalani rasilimali zinazokuzunguka ni ardhi, watu na maji, ni vipi mchanganyiko huu utautumia vizuri ili uweze kupata zao (output) ambayo itakusaidia kujikwamua katika hali uliyonayo. Ama ni vipi utatumia mtaji mdogo ulionao kufanya biashara itakayokuletea faida ambayo utaitumia kuongeza mtaji na kuikuza biashara yako.
 
Fahamu kwamba lengo lolote la mjasiriamali ni kupata faida na kumridhisha mteja ambaye anatumia bidhaa ama huduma inayotolewa na mjasiriamali. Bidhaa ama huduma ndio msingi wa mjasirimali yeyote ambaye anataka kupata faida. Mathalani mkulima wa mahindi bidhaa yake ni mahindi hivyo atauza mahindi kujipatia faida, na mtabibu wa mifugo anatoa huduma ya matibabu kwa mifugo na kulipwa ujira kwa kutoa huduma hiyo.
 
Itaendelea....
 
Niandikie: mmlanzi@yahoo.com