Pages

Thursday, May 30, 2013

Kinachodaiwa kumuua Msanii Mangwea hiki hapa

 
Dar es Salaam. Wakati mazishi ya mwanamuziki marehemu Albert Mangwea(28) maarufu kama `Ngwair’ yakitarajiwa kufanyika mjini Morogoro, maeneo ya Kihonda baada ya mwili kuwasili nchini, hospitali iliyomfanyia vipimo imethibitisha kuwa pombe na dawa za kulevya kupita kiasi ndivyo vilivyomuua.
Mwili wa mwanamuziki huyo, ambaye alitamba kwenye miaka ya 2000 na wimbo wa `Mikasi’, unatazamiwa kuletwa kesho nchini na kuagwa Jumamosi kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Kihonda, Morogoro kwa mazishi.
Kwa mujibu wa taarifa Mangwea alifariki dunia juzi kwenye Hospitali ya St Hellen, iliyopo Johannesburg, Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwa shughuli za muziki.
 
Kifo chake
Ripoti iliyochapwa na mitandao mbalimbali ya ndani na nje ya nchi inasema marehemu alifikwa na umauti baada ya kulewa kupindukia, kibaya zaidi alikuwa hajala.
Siku ya kifo chake, Mangwea alianguka nyumbani kwa rafiki zake akiwa katika hali hiyo ya kulewa sana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya kufikishwa hospitalini, Mangwea aligundulika kulewa mara tano ya kipimo cha kilevi kilichopitishwa na serikali ya Afrika ya Kusini, ambacho ni 416mg za pombe kwenye kila milimita 100(kwa mlevi anayeendesha chombo cha moto).
Pia marehemu alikutwa na upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye seli na tishu za mwili wake.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Mangwea, maarufu Ngwair, alikuwa na tatizo la kutokula chakula vizuri kabla ya kifo chake na pia kukosa muda wa kupumzika.

Sampuli zilizopatikana mwilini mwake zinaonyesha mkusanyiko wa dawa za kulevya mbalimbali zikiwemo heroine, cocaine chafu na bangi ya gramu 0.08 ambavyo vilikutwa kwenye damu yake.

Kifo chake kilitokana na mshtuko wa moyo na kushindwa kupumua, hali iliyosababisha mapigo ya moyo wake kusimama kwa sekunde chache, na kusababisha kifo chake.

Mwili wa Ngwair ulionekana kana kwamba alitokwa na damu nyingi puani baada ya kuonyeshwa kwa Watanzania wengi jana jioni Johannesburg, Afrika Kusini.

Taarifa za awali zilizotolewa na rafiki wa karibu aliyepo nchini Afrika Kusini, aliyejitambulisha kwa
 jina moja tu la Jonathan zilidai kuwa marehemu hakuamka tangu alipopumzika usiku wa kuamkia juzi.

Endelea: Mwananchi

Friday, May 24, 2013

Wamemdharau Nyerere na Kuivunja Misingi - Sasa hawana pa Kushikilia!



 
Kwao Nyerere siyo "Baba wa Taifa" tena; kwao ni "Mzee Nyerere"; kwa watawala wetu hawa walioshindwa wanasema wamefanya mambo mengi sana ya maendeleo kuliko "Wakati wa Nyerere". Wanajitamba kuwa wao wamekuza sana demokrasia na kuwa hata "Nyerere" hakuweza kufanya waliofanya wao. Katika upotofu wao wanaamini kabisa kuwa wao wanapendwa zaidi; na wanapendwa kwa sababu wamefanya mengi mno na hawaelewi kwanini watu hawaoneshi shukrani!

 Ndio maana kila kukicha hawaachi kubembeleza kwa wananchi kuwa "hamuoni tunayofanya" na kuwa watu wanalaumu tu lakini hawatoi pongezi kwa "mazuri mengi". Imefika mahali Kikwete mwenyewe amedai mahali fulani anataka kukumbukwa kuwa ni "bwana maendeleo"; anasema hivi kwa sababu anapokaa ofisini anaamini kabisa kuwa ameweza kuwapatia Watanzania 'vitu" vingi sana vya maendeleo kuliko wakati wowote wa historia - vitu ambavyo hata Nyerere hakuweza kuwapatia. Kikwete anataka awe juu ya Nyerere kwa kila kipimo kwani kipimo kilichowekwa ni Nyerere. Na bila ya shaka kuna sababu - Nyerere hakuamini kuwa walikuwa tayari kuwaongoza Watanzania - hawa kina Kikwete na Lowassa.

 Sasa katika kumdunisha Nyerere ili wao wakue wameacha propaganda chafu dhidi ya Nyerere na uongozi wake. Leo hii tunashuhudia mambo ambayo - pamoja na 'ubaya' wote wa Nyerere hayakuwahi kutokea chini ya "dhaalim Nyerere"! Matukio yanayotokea leo hii ukiwaambia watu walioshi wakati wa Nyerere, chini ya chama kimoja na uongozi thabiti hawawezi kuelewa yanawezekana vipi kutokea. Watu wa enzi za Mwalimu wanakumbuka vizuri kuwa kiongozi aliyefanya madudu hakuvumuliwa; na bahati mbaya wakati ule hatukuwa na wasomi wengi na watu wengi wenye udhoefu lakini Nyerere hakuwaonea huruma. Wapo ambao hadi leo wana kinyongo na Nyerere kwa sababu hakuwapa nafasi nyingine.

 Lakini katika kumdharaulisha Nyerere na kujaribu kupuuza mafanikio yake makubwa zaidi wamejikuta hawana pa kukimbilia! Tuliokuwa wakati wa Nyerere hatukumbuki jinsi JWTZ likitumiwa kisiasa kama linavyotumika hivi sasa! Fikiria ndege ya jeshi itumwe kumchukua raia kumpeleka Mahakamani!? Kwamba, ati vurugu za uchaguzi zilazimishe JWTZ kuingilia kati! Kwamba vikosi vya kutuliza ghasia vya polisi vizidiwe nguvu na mara moja kuliingiza jeshi kufanya kazi za jeshi la polisi! Unthinkable! Lakini wao wanaamini wako sawa!

 Lakini siyo kwamba wamedharaulisha na kumtupa nje Nyerere ni zaidi ya hivyo; wameitupa misingi ya taifa letu. Wanataka kujenga kwa misingi ya mabua! Waliachiwa misingi ya zege lakini wao wakiamini ni 'magenius" wameamua kutengeneza 'taifa jipya' nje ya misingi iliyounda Tanzania. Leo hii Watanzania kwa mamilioni wananung'unika moyoni kwani hawatambui kama hili ndilo Taifa waliloachiwa kama urithi. Sasa hivi inaonekana Tanzania inazidi kufanana zaidi na mataifa mengine ya Afrika kiasi kwamba linaweza lisitofautike tena mbele ya umma.

 Wameitupa misingi sasa hawana cha kujengea; wamebakia kutumainia vitisho, dharau na matumizi ya nguvu. Wameshindwa kabisa kujenga hoja - kwa mfano kwenye hili suala la gesi. Hawana ushawishi wa hoja na badala yake hata kauli zao wanazotoa zimejaa dharau (contempt) na matokeo yake watu nao wanawadharau! Wanafikiri vitisho na kejeli zinajibu hoja!

 Kushindwa kwa sera zao mbalimbali ni matokeo ya kuachana na misingi ya taifa; wanafikiri wanaweza kutengeneza sera nzuri nje ya misingi ya taifa! Matokeo yake:

 Sera ya Nishati na Madini imeshindwa

 Sera yao ya Gesi imeshindwa - hata kabla haijaanza!

 Sera yao ya Elimu imeshindwa
 Sera yao ya siasa imeshindwa
 Sera yao ya Sayansi na Teknolojia imeshindwa
 Sera yao Mazingira imeshindwa
 N.k

 Wameshindwa lakini hawaamini wameshindwa na badala yake wanawalaumu wanaowaambia wameshindwa kwa kushindwa kwao! Kana kwamba, wanaowalaumu wakinyamaza basi wao wataweza! Wenyewe wanaambizana kuwa wakipewa nafasi nyingine 2015 basi wataaanza kuweza; na wapo watu wanaamini kuwa hilo linawezekana; kwamba pundamilia anaweza kugeuka na kuwa farasi! Kama wenyewe wameshindwa kuvuana magembe licha ya mbwembwe zote za "kuvuana magamba" kweli kuna uwezekanow wataweza? Na ukweli ni kuwa walipofika sasa hawawezi kurudi kwenye misingi ya Nyerere na Taifa letu; kwa sababu kurudia misingi hiyo ni kujishtaki katika historia.

 kuna namna moja tu ya kuwasaidia... kuendelea kuwakataa.

 Maskini CCM! 
 Maskini Kikwete
 Maskini Tanzania chini yao!
Source: Mwanakijiji

Wednesday, May 22, 2013

Bajeti nishati

 
Dodoma/Mtwara.
Wakati mjadala mkali ukitarajiwa kuibuka bungeni leo wakati Serikali itakapokuwa ikiwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, joto limezidi kupanda mkoani Mtwara ikielezwa kuwa wananchi wamehamasishana kwa mara nyingine kuacha shughuli zote ili kusikiliza kama hotuba hiyo italinda masilahi yao.
Hotuba hiyo ambayo itasomwa leo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, inatarajiwa kuibua mengi yakiwamo yanayohusu suala la gesi ya Mtwara.
 
Mjini Mtwara vipeperushi vinavyopingana vilisambazwa kuhamasishana ‘kuacha shughuli zao zote na kubaki nyumbani ili kufuatilia matangazo ya televisheni wakati Profesa Muhongo atakapotangaza bajeti hiyo, huku vingine vikipinga.
 
Ahadi za matumaini
Licha ya kampeni hizo za watu wa Mtwara, Serikali nayo imeweka matangazo katika vyombo vya habari likiwemo gazeti hili ikieleza namna mikoa ya Mtwara na Lindi itakavyonufaika na utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia.
Tangazo lililotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania limeainisha faida za gesi hiyo kwa Mkoa wa Mtwara ukiwamo umeme utakaotokana na gesi asilia. Pia imeelezwa jinsi mafunzo kwa vijana juu ya matatizo ya gesi asilia yaliyodhaminiwa na Wizara ya Nishati na Madini na kampuni mbalimbali kuanzia mwaka 2010.
Vilevile imeelezwa jinsi uboreshaji wa huduma za jamii kama ujenzi wa shule, hospitali na ujenzi wa viwanda kama kile cha saruji cha Dangote na mitambo ya kusafishia gesi utakavyowanufaisha wakazi wa mkoa huo.

Gesi hiyo ambayo pia inachimbwa katika Kisiwa cha Songosongo inatajwa kwamba itawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Lindi kwa kupata umeme, kunufaika na kodi ya wawekezaji wa gesi na udhamini wa mafunzo kutoka kampuni mbalimbali na wizara.
Wiki iliyopita Profesa Muhongo alijigamba kuwa bajeti ya wizara yake atakayosoma leo itakuwa ya karne ya 22 itakayomaliza tatizo la umeme nchini kwa kuwa imetoa vipaumbele kwa sekta binafsi kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Wabunge wapania
Dalili za kuibuka mjadala mkali katika bajeti ya leo zilianza kujitokeza mwishoni mwa wiki wakati wa semina ya wabunge kuhusu masuala ya gesi ambapo wizara hiyo ilibanwa juu ya mambo ya mikataba.
Hata hivyo, semina hiyo ilitafsiriwa kuwa ililenga kuwapoza wabunge na kupunguza hasira zao huku wizara ikijipanga namna ya kuwashawishi waikubali bajeti baada ya kuona mwelekeo wao.

Wasiwasi Mtwara
Hali ya wasiwasi imeanza tena kutanda mkoani hapa hasa kutokana na vipeperushi vinavyokinzana na ujumbe tofauti kwa njia ya simu unaosambazwa.
Hali hiyo imejirudia tena huku ikionekana dhahiri kuwa na kauli kutoka makundi tofauti zinapishana katika vipeperushi hivyo huku wengine wakitaka mwendelezo wa kusitisha huduma ufanyike na wengine wakipinga.
Mojawapo ya kipeperushi kilisisitiza huduma zote zisitishwe kuanzia bajaji, bodaboda, masoko na magari yote yaendayo mikoani na wilayani yasiingie wala kutoka.
 
Huku vipeperushi vingine vikipinga: “Tunafahamu gesi ni mali yetu wote Wanakusini na tunafahamu kunyanyasika kwetu na Serikali ya nchi yetu na Mei 17 tuliunga mkono kufunga maduka na biashara zote, lakini hatukunufaika na chochote.
“Sasa Jumatano tena tusifanye biashara. Tuache ujinga Wanakusini wenzetu wengine hawana kazi wala gesi. Kampeni zitafanya tuwe maskini zaidi. Tarehe 22.05.2013 hatufungui duka wala hoteli, hata soko,” kilisomeka kimoja kati ya vipeperushi hivyo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Linus Sinzumwa aliwataka wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku bila kujali vitisho hivyo kwa kile alichokidai kuwa ulinzi umeimarishwa.

mwananchi

Wednesday, May 15, 2013

Kumwongezea JK muda

 
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amedai kuwa amenasa taarifa za siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani.
Profesa Lipumba alisema hiyo inatokana na wasiwasi kuwa mchakato wa Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014 hivyo kutokuwa rahisi kwa uchaguzi kufanyika mwaka 2015.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la CUF, Profesa Lipumba alisema kuwa Serikali inataka kuongezewa muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili ikimaanisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete itakaa madarakani hadi mwaka 2017.
 
Hata hivyo, madai hayo ya Profesa Lipumba yamepingwa vikali na Serikali na viongozi wake watatu waandamizi ambapo walijibu walipoulizwa kwa maandishi na mwandishi wetu mjini Dodoma wanakohudhuria kikao cha Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alijibu: “Mchakato wa Katiba upo ‘on track’ (unakwenda vizuri) hatuna sababu ya kufanya hivyo.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijibu” “Njooni ofisini kwangu nitasema ni kitu gani.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alijibu kwa utani bila ya kufafanua: “Njooni niwajuze, unajua kamba haitoki Ukambani kama ilivyo kamba.”

Profesa Lipumba amemwomba Rais Kikwete asilikubali wazo hilo akisema wananchi hawatakubali na taifa linaweza kuingia katika mtafaruku.

“Nitapenda kuona Rais Kikwete akikataa jambo hilo kwani litachafua taswira ya nchi. Hatua hii ni kinyume cha utawala bora,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema Serikali haipaswi kuhofia uchaguzi kwa sababu ya Katiba kwani bado uwezekano wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru unawezekana kwa utaratibu mwingine.

“Mchakato wa Katiba unaendelea, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatuambia kwamba mwaka 2014 tutakuwa na Katiba Mpya, sasa CUF tunasema kwamba hata kama Katiba Mpya haitapatikana kwa kipindi hicho kuwe na Tume huru ya Uchaguzi,” alisema Profesa Lipumba.

source:mwananchi

Friday, May 10, 2013

‘Mkutano wa amani ni ‘porojo’: Mtikila

 
Dar es Salaam. Wakati Mkutano wa Viongozi mbalimbali wa dini na Jeshi la Polisi ukimalizika jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema mkutano huo ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick, umejaa porojo na kwamba hauwezi kuleta suluhu yoyote.
Kwa siku mbili, viongozi hao wa kidini walikuwa wakijadili masuala ya amani ya nchi baada ya kutokea tofauti mbalimbali pamoja na kuwapo mazingira ya kuhatarisha amani nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana akiwa nje ya ukumbi wa mkutano huo, alisema kwa kawaida imani ya mtu ipo ndani ya roho yake na huwezi kuiondoa kwa maneno au kufanya mikutano bali kinachotakiwa ni Serikali kujitahidi kuondoa makosa yaliyojitokeza siku za nyuma ambayo ndiyo yamezaa tofauti zinazojitokeza.
                              
“Mimi nadhani mkuu wa mkoa na chama chake kukaa na kufikiria kuitisha mkutano wa viongozi wa dini wenye lengo la kumaliza tofauti za dini ambazo zinajitokeza haupo sahihi kwani ni vyema tatizo likaangaliwa lipo wapi ili kupata majibu sahihi ya tofauti zinazojitokeza sasa,” alisema Mtikila. Mkutano huo ulitarajiwa kufungwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.

Alisema katika mkutano huo hakutakuwa na suala jipya kwani kila kitu kipo wazi na kwamba tatizo linalojitokeza wakati huu ni la muda mrefu tangu mwaka 1986 ambapo aliwahi kusema masuala ambayo yatakuja kujitokeza siku za usoni ikiwamo suala la udini.

“Mimi nadhani kwamba kuna haja ya msingi kuangalia suala hili la imani za kidini kwa undani hasa kutafuta tatizo lipo wapi,lakini siyo mtu mmoja akae na na kufanya mkutano kwa lengo la kutafuta suluhu ya migogoro ya dini wakati si jambo rahuisi kiasi hicho,”alisema.

Source: Mwananchi
 
 

Wednesday, May 8, 2013

Bomu Arusha: Pengo afichua siri


Dar es Salaam/Arusha. Kadinali Pengo alisema amepata taarifa kutoka kwa watu ambao hana na shaka nao.

“Jana (juzi), niliongelea kwamba suala zima la tukio la Arusha halihusiani na imani yoyote ya kidini. Tamko hilo nilitamka kutokana na taarifa nilizofikishiwa na watu ambao sikuweza kuwa na shaka kwamba wanaoniambia ni kweli na sidhani kama ningekuwa na sababu ya kusema wamefika kwa kunidanganya kwa hiyo tamko litakuwa limesimama juu ya msimamo huo,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza:

“Lengo la msingi kabisa, langu na la kanisa ni kwamba tukio lolote lile liwe kwa nia mbaya au nzuri kwa upande wetu isiwe ni sababu ya kuanza mapambano na kuwa chimbuko la ukosefu wa amani katika nchi yetu,” alisema Pengo.
 
Alisema kuwa kila anayehusika ajue amani ya kweli ya taifa lolote haiwezi ikapatikana isipokuwa ikijengwa juu ya ukweli na ukweli kabisa bila kufuta au kujaribu kupotosha ukweli kwa namna yoyote ile.

“Tusipojua kusema ukweli ulivyo hatuwezi kufaulu kuleta amani katika taifa letu. Kwa hiyo pamoja na kuendelea kuwaomba waumini wa Katoliki pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu arehemu taifa letu na mapambano ya aina yoyote ile. Tuendeleze nia yetu njema ya kusema ukweli, haidhuru ukweli huu unamgusa nani,” alisema Pengo.
 
Alisema kujaribu kuficha ukweli na kupotosha ni njia sahihi kwa ibilisi kuleta vurugu katika jumuiya ya watu na ieleweke hivyo.

“Naomba kila mtu akubaliane na tamko langu haidhuru pana kosa, amani ya taifa letu ni jambo la msingi na amani itajengwa tu iwapo kila mtu anayehusika atakuwa tayari kusema ukweli kama ulivyo,” alisema.

Mwingine afariki, 20 wakutwa na vipande vya chuma miilini
Katika hatua nyingine, majeruhi mmoja katika shambulio hilo lililotokea Jumapili iliyopita, amefariki dunia juzi jioni na kufikisha idadi ya waliopoteza maisha kufikia watatu.

Aliyefariki ni mtoto wa miaka tisa, Patricia Joachim ambaye alikuwa amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi. Wengine waliofariki katika tukio hilo ni Regina Losyoki (45) na James Gabriel (16).

Mazishi ya watu hao watatu yamepangwa kufanyika katika eneo la kanisa hilo Ijumaa.
Katika hatua nyingine, majeruhi 20 wamebainika kuwa na chembechembe za vyuma walivyopata katika shambulio hilo. Hao ni miongoni mwa majeruhi 42 waliolazwa hadi sasa kwenye hospitali mbalimbali za Arusha.
 
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Thomas Kway alisema majeruhi hao 20 wamedhuriwa na chembechembe za vyuma vya mabomu na baada ya miili yao kubainika kuwa na vyuma vyenye urefu hadi wa sentimita tisa.

Dk Kway alisema hayo wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipofika katika hospitali hiyo kuwafariji majeruhi hao.

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliwataka madaktari waliowafanyia upasuaji majeruhi waliolipuliwa na bomu kuhifadhi vipande hivyo ili vitumike katika uchunguzi.

Aliwaambia wabunge kuwa vyuma hivyo vitasaidia upelelezi ili kufahamu aina ya bomu lililotumika.
“Tumeamua kuwa vipande vya vyuma vinavyotolewa baada ya upasuaji visitupwe, vitumike kwa uchunguzi,” alisema Pinda na kuongeza kuwa baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
 
Waliokamatwa
Akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alifika Arusha jana, Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema watu tisa wamekamatwa hadi sasa.

Aliwataja baadhi yao kuwa ni Victor Ambrose na wengine aliowataja kwa jina mojamoja ni Joseph na David.

Alisema wengine ni raia watatu wa Saudi Arabia, ambao walikuwa na wenyeji wao wawili na Watanzania wengine watatu.

Kauli ya Kikwete
Akizungumza Arusha jana, Rais Kikwete amewataka waumini wa dini zote waendelee kusali akiahidi kwamba Serikali itaimarisha ulinzi. Alisema amekerwa na kukasirishwa na tukio hilo.

Rais Kikwete alitanguliwa kufika Arusha na Makamu Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ambao pia walitembelea Kanisa lililolipuliwa na baadaye kwenda kuwatembelea wafiwa na kuwafariji majeruhi hospitali.

Viongozi wote hao walitoa wito kwa Watanzania kulinda amani iliyopo na kuacha malumbano ambayo hayana tija kwa maslahi ya taifa.
Chanzo: Mwananchi

Tuesday, May 7, 2013

CCM ndio chanzo cha Udini: Zitto


Mbunge wa Kigoma kaskazini na naibu katibu mkuu wa CHADEMA mh Zitto Kabwe jana alikituhumu wazi wazi Chama Cha Mapinduzi kuwa ndio kiini cha udini unaoanza kuligubika taifa la Tanzania lililokuwa linasifika kwa amani.
 
Akichangia hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara ya mambo ya Ndani jana usiku Bungeni mjini Dodoma, Zitto alisema CCM imekuwa na tabia ya kuvihusisha vyama vya upinzani vyenye nguvu na udini. "Wakati chama cha wananchi CUF kilipokuwa na nguvu kilihusishwa na dini ya kiislamu, vivyo hivyo kwa CDM ambacho kinahusishwa na dini ya kikristo pamoja na ukanda" alisema Mh Zitto.
 
"Hali hii bila kujua ndi imeleta mifarakano ya kidini miongoni mwa jamii yetu hivyo kupelekea kuwa na chuki kubwa miongoni mwa dini hizi mbili na kusababisha matukio ya ajabu kutokea katika nchi yetu" Alisema Mh Zitto.
 
Hata hivyo Zitto kwa kiasi kikubwa aliwalaumu viongozi wote kwa ujumla kuacha kutoa hotuba zenye kuchochea chuki miongoni mwa jamii ya Tanzania na kubadilika mara moja ili kuijenga upya jamhuri ya muungano wa Tanzania ambayo kwa sasa ina nyufa nyingi zinazoweza kuliangusha taifa hilo nguli la Amani.

Wasaudia wanne mbaroni, FBI watua Arusha


Dodoma/Arusha. Wakati maofisa wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (FBI) wametua Arusha, raia wanne wa Saudi Arabia na Watanzania wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika kulipua bomu lililoua watu wawili na kujeruhi wengine 61 wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti.

Waliofariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45), mkazi wa Olasiti na James Gabriel (16), ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo lilitokea wakati Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini, Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizindua kanisa hilo.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema raia hao wa Saudi Arabia walikamatwa jana asubuhi baada ya tukio wakiwa kwenye gari wakielekea Kenya kupitia Namanga.

Mulongo alisema raia hao wa kigeni waliingia nchini Jumamosi iliyopita na siku iliyofuata ndipo kukatokea ulipuaji huo. Alisema lengo la shambulizi hilo lilikuwa kumdhuru Askofu Padilla.
 
“Mtu ambaye tulimkamata jana (juzi Jumapili) ndiye aliyesaidia kuwapata watu hawa wa Saudi Arabia na Watanzania hao,” alisema Mulongo.

Mulongo alisema maofisa wa FBI walifika jana saa tano asubuhi ili kusaidiana na Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika uchunguzi wa tukio hilo.
Maofisa hao wa FBI walikuwa Zanzibar ambako walikuwa wanachunguza kifo cha Padri Evaristus Mushi ambaye aliuawa Februari 17, mwaka huu.

Hii itakuwa mara ya pili kwa wageni kuhusishwa na matukio ya ugaidi nchini baada ya mwaka 1998 wakati raia kadhaa wa Misri wakiongozwa Fazul Abdulla waliposhirikiana na Watanzania kadhaa akiwamo Ahmed Ghailani kulipua ubalozi wa Marekani nchini na ule wa Kenya. Ghailani anatumikia kifungo cha maisha nchini Marekani wakati Fazul aliuawa Somalia mwaka 2011.

Tamko la Serikali
Akitoa tamko la Serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alimtaja mmoja wa watuhumiwa wanaoshikiliwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Victor Calisti Ambrose (20), mkazi wa Kwa Mrombo Arusha ambaye ni dereva wa bodaboda. Alisema kijana huyo ndiye anayetuhumiwa kurusha bomu hilo.

Waziri Nchimbi alitoa onyo kali kwa wanasiasa wanaopandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kuishutumu Serikali kutokana na matukio kama hayo. “Kuna wanasiasa ambao wanaona masilahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania, masilahi yao ni muhimu kuliko utulivu wa Watanzania na masilahi yao ni muhimu kuliko umoja wa Watanzania.”
 
JK akatiza ziara, Bilal atoa ahadi
Rais Jakaya Kikwete, amekatiza ziara yake ya kiserikali nchini Kuwait ili kurejea nyumbani kutokana na shambulio la bomu kwenye kanisa hilo.

Taarifa ya Ikulu imesema jana kwamba Rais Kikwete amelazimika kukatiza ziara hiyo na kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ameahidi kuwa Serikali itahakikisha wote waliohusika na tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Balozi wa Papa atoa tamko
Askofu Padilla ambaye jana alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Mkoa, Mount Meru, alieleza kustushwa na tukio hilo na kusema hakutarajia kitu kama hicho kutokea wakati wa shughuli hiyo wakati Watanzania wakijulikana ni watu wa amani.
Alilaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.

Kanisa Katoliki Arusha
Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha jana liliitaka Serikali iwataje waliohusika na tukio hilo la kigaidi huku likiwataka waumini wake kutolipiza kisasi.

“Msimamo wa kanisa katika hili, ni kuwataka waumini wasilipize kisasi kama ambavyo alisema Yesu Kristo kuwa msilipize kisasi, muwe tayari kushinda ubaya kwa wema,” alisema Askofu Josephat Lebulu na kuongeza:
EU
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), imetaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa tukio hilo na kuonya kuwa matukio kama hayo yanaweza kulitumbukiza taifa kwenye machafuko.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Umoja huo nchini, Filiberto Ceriani-Sebregondi alisema Tanzania inapaswa kufahamu kwamba pasipo kujenga, kuendeleza na kusisitiza utamaduni wa kuvumiliana, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa siku za usoni.
 
Source: Mwananchi