Pages

Friday, August 31, 2012

Bashe, Kigwangallah katika vita ya bastola


BASHE AMTUHUMU KIGWANGALLAH KUMTISHA KWA SILAHA,NAYE AENDA POLISI KUWATUHUMU WAFUASI WA BASHE KUMTISHA


Waandishi Wetu

VITA ya mahasimu wa siku nyingi katika siasa wilayani Nzega, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangallah imechukua sura mpya, baada ya makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufikia hatua ya kutishiana kwa bastola hadharani.Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Bashe na Kigwangallah kwa nyakati tofauti kila mmoja amekanusha madai hayo akimtuhumu mwenzake kuwa ndiye aliyekuwa na silaha.



Wakati Bashe akisema Dk Kigwangallah ambaye pia ni mbunge wa Nzega ndiye aliyetoa bastola kumstishia wakiwa ndani ya ofisi ya ya CCM Wilaya, Dk Kigwangallah anaeleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi ambao wanalifanyia kazi.



Habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa, Dk Kigwangallah na Bashe walizua tafrani hiyo juzi wakati wakirejesha fomu za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wilaya ya Nzega.



Upinzani baina ya wanasiasa hao vijana, ulianza 2010 baada ya Kigwangallah kupitishwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura za maoni, ndani ya chama hicho.



Bashe ambaye aliibuka kidedea katika mchakato huo wa kura za maoni alitoswa na chama hicho kwa maelezo kuwa hakuwa raia wa Tanzania, huku aliyeshika nafasi ya pili, Lucas Selelii ambaye alikuwa kinara wa kupambana na mafisadi wa chama hicho naye akitoswa. Baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Lawrence Masha alisema Bashe alikuwa raia halali wa Tanzania.



Vita hiyo ilionekana kuendelea juzi baada ya kudaiwa kutishiana bastola huku kila mmoja akitoa maelezo ya kumrushia lawama mwenzake.



Ilivyokuwa

Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyehoroka alisema Bashe alifika ofisini hapo kurejesha fomu saa 09:50 alasiri, muda mfupi baada ya Dk Kigwangallah ambaye alifika saa 09:48.



“Kigwangala alifika na kuingia ofisi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Fransis Shija, ambako alikaa na kujaza fomu yake. Bashe naye alifika akaingia ofisini kwangu, akakaa na kuandika," alisema.



Katibu huyo aliendelea kueleza kuwa ilipofika saa 9:55, Dk Kigwangallah alikwenda kwa katibu muhutasi kurejesha fomu yake na kukaa hapo.



"Bashe alipofika hapo naye alisimama akingoja Kigwangallah amalize, lakini Kigwangallah alimueleza kuwa muda wa kurejesha fomu umemalizika, hivyo kumzuia kurudisha fomu, hali iliyozua mvutano na vurugu" alieleza katibu huyo.



Katibu wa Vijana wa CCM Wilayani Nzega, Salome Nyombi, alisema baada ya vurugu hizo kuzuiliwa ndani ya ofisi ya katibu, Bashe alitolewa nje ambako alianza kuwasimulia rafiki zake kilichotokea ndani.



Alisema baadaye Kigwangallah naye alifika eneo hilo na kuanza kurusha maneno, hali iliyozua mtafaruku mwingine katika eneo hilo.



"Alipozuiliwa kufanya vurugu, aliendelea kutukana na kisha kutoa bastola akiwatishia watu waliokuwa wakizungumza na Bashe kwa madai kuwa ni vibaraka wake," alisema na kuongeza:



“Hali ilikuwa mbaya kiasi cha baadhi yetu kulazimika kukimbia, na wengine tulilala kwenye viti, lakini kijana mmoja anayeitwa Sango, alimzuia (Kigwangallah) kwa kujaribu kumpiga kwa kiti, ndipo watu walipomtoa Bashe na kumpeleka eneo lingine.”



Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wilayani Nzega, Mary Igogo, alisema amesikitishwa na vurugu hizo na kusema iwapo wasingemzuia Bashe, kungezuka ugomvi mkubwa.



Katibu CCM mkoa

Katibu CCM Mkoa wa Tabora, Iddi Ame akizungumuza kwa simu, alisema ndani ya CCM ni ajabu kwa wanachama kutishina kwa silaha.



Ame alisema kuwa kitendo hicho ni aibu kubwa kwa CCM huku akiuagiza uongozi wa Wilaya ya Nzega kutoa maamuzi mapema juu ya vurugu za makada hao.



“CCM hatuna historia ya kutishana kwa bastola na kamwe jambo hilo haliwezi kuwa siasa kwa kuwa linaleta sura mbaya ndani ya chama chetu, nawaagiza uongozi wa wilaya watoe tamko au maamuzi ya jambo hili mapema,”Ame.



Shuhuda

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alisema vurugu zilikuwa kubwa zaidi nje ya ofisi za CCM baada ya mahasimu hao kutolewa ndani ya ofisi hizo baada ya kuanza kulumbana.



Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zilieleza kuwa Kigwangallah alifika katika kituo cha polisi na kufungua malalamiko ya kutishiwa maisha na Sango Issaya, Hussein Bashe pamoja na Majaliwa Bilali.



Taarifa hizo zilifafanua kwamba kwa nyakati tofauti mahasimu hao walitoa maelezo yao polisi na wapo nje kwa dhamana mpaka pale upelelezi wa tuhuma walizopeana utakapokamilika.



"Tumepokea taarifa za hawa watu na tunaendelea na upelelezi wetu mpaka hapo tutakapojiridhisha na ushahidi ndipo tutawapeleka mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,”alisema ofisa mmoja wa polisi wa ngazi za juu wilaya.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Antony Rutta, aliliambia gazeti hili kuwa taarifa za tukio hilo alizipata, lakini anaendelea kuzifuatilia kujua chanzo chake.



“Ni kweli nimepata taarifa za Bashe na Kigwangallah wamedaiwa kutishiana bastola…mimi nilisikia hayo nikiwa njiani kutoka huko Nzega kurudi Tabora….nitafuatilia,”alisema.



Kauli za Bashe, Kigwangallah

Bashe alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akakanusha kumtishia bastola Dk Kigwangallah akidai kuwa mwenzake huyo ndiye aliyemtishia yeye kwa bastola akitaka fomu yake isipokelewe kwa kile alichoeleza kuwa imechelewa kurejeshwa.



“Huyu ndugu yangu ana visa na chuki dhidi yangu, ni kweli alinichomolea bastola, lakini wanachama walituamulia," alisema



Hata hivyo, Bashe alieleza kuwa pamoja na hila hizo, Dk Kigwangallah hamuwezi kisiasa kwani katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika zikiwahusisha wao, amekuwa akimshinda kwa kishindo.



"Kigwangallah pia aliwahi kuvamia mkutano wangu, lakini niliwaambia watu wangu wamwache. Anachotafuta ni confrontation (msuguano) na mimi ili kutokee tatizo nienguliwe kwenye uchaguzi baada ya kuona haniwezi," alisema.



Bashe alisema kwamba amegundua Kigwangallah anatumia mbinu ili majina yao yakatwe yote kwa kuwa ameshaona hawezi kumshinda. “Jamani Kigwangallah hawezi kunishinda, amenitishia na bastola nikakaa kimya, sikupenda kabisa kumjibu maana najua anachotafuta,” alisema



Kwa upande wake, Dk Kigwangallah alisema aliomba Bashe azuiwe kurejesha fomu yake kwa kuwa aliirudisha nje ya muda, lakini alishangaa kuona anafanyiwa vurugu na wafuasi wake.



Alisema alitishiwa maisha na watu watatu ambao aliwataja akiwamo Bashe na kueleza kuwa tayari malalamiko hayo ameyafikisha polisi.



"Walinzi wa Bashe ndio walionitishia bastola na baada ya tukio hilo nikaenda kuripoti polisi na tayari polisi wamechukua hatua ikiwamo kuwafikisha mahakamani Bashe na wapambe wake hao," alisema Dk Kigwangallah na kuongeza;



“Huyu ndugu yangu (Bashe) ni mzushi anataka kuyakuza mambo tu. Katika hilo Katibu amembeba kwani muda wa kurejesha fomu ulikuwa umeisha".

Alisema Bashe amekuwa akijaribu kumfanyia faulo ya kumtishia huku akitembea na jopo la waandishi wa habari ili wamchafue.



’’Nimeamua kuja kutoa taarifa kwani nimetishiwa maisha yangu na kijana huyu pamoja na Bashe lazima nitoe taarifa hizi, maana nimeonewa,’’alisema Kigwangallah.



Alipoulizwa kana anamiliki bastola, Kigwangallah alisema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akimiliki silaha hiyo.



“Kama ningeamua kuua ningeweza kufanya hivyo ila naelewa maana ya kuwa na silaha ya moto, ndio maana nimekuja hapa kutoa taarifa kwa sababu lolote linaweza kutokea” alisema mbunge huyo wakati akiwa Kituo cha Polisi Nzega.



Zungu amkacha Mkono

Katika hatua nyingine mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ameshindwa kurudisha fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa Wazazi Taifa.



Siku ya mwisho ya kurejesha fomu ilikuwa juzi, lakini mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge alishindwa kuirejesha kama walivyofanya wagombea wengine 16 akiwemo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.



Hastin Liumba, Frederick Katukanda, Nzega, Daniel Mjema, Moshi na Joseph Zablon, Dar

Source: Mwananchi

Dk Slaa amvutia pumzi Samuel Sitta


Mwandishi Wetu


KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni nzito, hivyo anajipanga kuijibu.
Dk Slaa aliliambia gazeti hili jana kuwa asingependa kuzungumzia kauli hiyo sasa kwa kuwa yuko ziarani vijijini, lakini ataitolea tamko wakati mwafaka ukifika.Habari ambazo baadaye gazeti hili lilizitapa zinasema kuwa Dk Slaa huenda akamjibu Sitta leo, atakapokutana na waandishi wa habari mjini Iringa.

 
Dk Slaa mwenyewe jana jioni alithibitisha kwamba atakutana na waandishi wa habari leo mjini Iringa, lakini hakuwa tayari kueleza kama atazungumzia kauli ya Sitta au la.

 
Kauli ya Dk Slaa imekuja baada ya gazeti hili kumtaka azungumzie kauli ya Sitta kuwa muda wa Chadema kutawala nchi bado, kwa kuwa chama hicho hakina viongozi makini wa kufanya kazi za Serikali.

 
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana Dk Slaa alisema,"Nimemsikia, lakini sijamwelewa. Naomba nipate muda wa kusoma vizuri alichosema, halafu nitamjibu tu."

 
Aliendelea:"Mimi sasa nipo huku Mufindi, sina mawasiliano yoyote ya msingi, naomba nipate muda zaidi wa kujiridhisha maneno yake kabla sijamjibu, nikiwa tayari nitawajulisha (waandishi).”
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza na gazeti hili jana alisema mkutano wa Dk Slaa na waandishi wa habari utalenga kueleza jinsi Chadema kinavyoendesha Operesheni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), baada ya kuzuiwa kwa mikutano yake ya hadhara.

“Kwenye mkutano na wanahabari, mambo mengi yanaweza kutokea. Kwa hiyo siwezi kukujibu moja kwa moja kama hilo unaloulizia (kauli ya Sitta) nalo litajibiwa au la,”alisema Makene.

 
Sitta alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera juzi, alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi ya Chadema, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake wana baadhi ya watu wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki.

 
Sitta alisema ukimwondoa Dk Slaa, hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza na kukifanya chama hicho kikubalike kwa umma.
“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanae Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri,” alisema Siita na kuongeza:

 
“Wote hapa mnasikiaga kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”
Kuhusu M4C
Katika hatua nyingine, Dk Slaa alizungumzia Operesheni inayojulikana kama M4C akisema Chadema imewabwaga polisi, kutokana na chama hicho sasa kubuni mbinu nyingine ya kujiendesha.
"Tuko huko Mufindi tunajenga chama, vikao kila wakati," alisema Dk Slaa alipoulizwa yuko wapi na anafanya nini.
Dk Slaa alisema CCM na Serikali yake, itajuta kuzuia mikutano ya hadhara ya Chadema kwani baada ya uamuzi huo, chama hicho kimekuja na njia nyingine ya kujijenga maeneo ya vijijini.
"Hawa watajuta (CCM na Serikali) kuzuia mikutano yetu. Sisi tumekuja na njia nyingine ya kukijenga chama vijijini," alisema Dk Slaa ambaye hata hivyo, hakubainisha njia gani anayotumia sasa kukijenga chama hicho cha upinzani.
Alipoulizwa atamaliza lini ziara yake hiyo ya kukijenga chama kwa njia mbadala, alijibu," Tulipanga kutumia siku 44 katika mikoa mitano, lakini nadhani siku hizo zitaongezeka baada ya mikutano yetu kuzuiwa.”
Mwanzoni mwa mwezi huu, Chadema kilianza ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini katika kile wanachokiita Movement for Change (M4C).
Hata hivyo, wakiwa mkoani Morogoro, chama hicho kiliingia katika mgongano na polisi katika vurugu zilizosababisha kifo cha mfuasi wake mmoja na majeruhi wawili.
Baadaye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Said Mwema aliipiga marufuku mikutano na maandamano ya chama hicho iliyopangwa kufanyika mkoani Iringa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupisha Sensa ya Watu na Makazi.



Source: Mwananchi

Thursday, August 30, 2012

Taarifa

Hii ni kuwaatarifu kuwa, blog yenu muipendayo itaendelea kutoa taarifa mbalimbali kama kawaida na siku za mapumziko, nitakuwa nawaletea taarifa za michezo na burudani kutoka katika vyanzo mbali mbali vya habari.


Karibu tuendelee kupashana Habari

Sitta: Tishio Chadema ni Dk Slaa tu

ADAI WENGINE NI WAZOEFU WA KUONGOZA KUMBI ZA MUZIKI, ATAMBA CCM KINA ZAIDI YA WATU 20 WENYE SIFA ZA URAIS, ZITTO AMJIBU


Edwin Mjwahuzi, Karagwe

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Samuel Sitta amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akidai kuwa muda wake wa kutawala nchi bado, kwa kuwa hakina viongozi wa kutosha wa kufanya kazi za Serikali ukimwondoa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.


Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Karagwe, Kagera, alikokuwa katika ziara ya kutembelea ofisi za CCM.


Alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi wa chama hicho, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake akidai kuwa kina baadhi ya viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki.Wote hapa mnasikia kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.


Dk Slaa na Mbowe hawakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Sitta baada ya taarifa kueleza kuwa Mbowe yuko nje ya nchi na alikuwa hapatikani kupitia simu yake ya mkononi kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa.


Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipinga kauli hiyo akimtaka Sitta aachane na chama hicho kikuu cha upinzani na atumie muda wake kukijenga chama chake ambacho alidai kuwa kina makundi zaidi ya sita.


Mwaka 2005 tuliweka mgombea Mbowe, mwaka 2010 tukamweka Dk Slaa, mwaka 2015 anaweza akarudi Mbowe, Dk Slaa au mwanachama yeyote wa Chadema, alisema Zitto.


Alisema Chadema ni taasisi na si chama cha makundi kama ilivyo kwa CCM hivyo hakiwezi kumtegemea mtu mmoja..Sitta asigombane na Chadema, ajenge chama chake ili tukutane mwaka 2015.


Akizungumza na viongozi hao wa CCM Karagwe, Sitta alisema hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza Chadema na kukifanya chama kikubalike kwa umma.


Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanaye Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri.


Kuhusu CCM

Akizungumzia chama chake, Sitta aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kutokaa kimya na badala yake wajitoe na kujibu hoja za upinzani wanazozitoa kuikosoa Serikali iliyopo madarakani ili ionekane haijafanya mambo ya maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru.


Serikali ya CCM imefanikiwa katika maeneo mengi ya huduma za jamii kama elimu, barabara, afya na mawasiliano, sasa inashangaza kuona viongozi wa chama mnashindwa kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera na ilani ya chama chetu.


Sitta aliwataka viongozi chama hicho nchini kuepuka mapambano na chuki miongoni mwao lakini akasisitiza kwamba kinaendelea na mkakati wake wa kuwaondoa viongozi wanaodaiwa kuwa ni mafisadi maarufu kwa jina la magamba.

Alisema chuki na mapambano yanayoendelea ndani ya chama hicho ndiyo yanayochangia kukidhoofisha na kuwapa la kusema wapinzani na hata kusababisha baadhi ya wanachama kukihama.


Mapambano ndani ya CCM ndiyo chanzo cha migogoro na mitafaruku inayosababisha viongozi na wanachama wetu kuombeana mambo mabaya na kutoa mwanya kwa watu wetu kuhamia upinzani.


Sitta yupo katika ziara ya siku tano ya kiserikali mkoani Kagera kukagua miradi mbalimbali inayohusiana na mwingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Source: Mwananchi

Sunday, August 26, 2012

Chadema yatingisha Igunga

YAFANYA MKUTANO MKUBWA IGUNGA KUSHUKURU WAPIGAKURA,DK SLAA AIONYA CCM IKIKATA RUFAA ITAUMBUKA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilitikisa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ikiwa ni mara ya kwanza tangu Mahakama Kuu Kanda Tabora kutengua ubunge wa Dk Dalaly Kafumu wa Chama Cha Mapinduzi, huku kikiionya CCM kuwa kitaumbuka iwapo kitakata rufaa kwa uamuzi huo wa mahakama.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Sokoine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema CCM kisithubutu kukata rufaa kwani kitaumbuka kwa kuwa kilicheza faulo nyingi katika uchaguzi huo.

Alisema ameshangazwa na kauli ya CCM kusema kuwa kitakata rufaa katika kesi hiyo wakati kisheria, kwa kesi za uchaguzi na pia katika hatua hiyo chama hakina nafasi yoyote bali mgombea au mwanachama wa chama husika, ndiye anayeweza kwenda mahakamani kufungua kesi na kupinga.

Katika mkutano huo uliofurika maelfu ya wanachama na washabiki wa wa chama hicho, Dk Slaa alisema kuwa Chadema kitakiangusha vibaya CCM hata ikiwa uchaguzi katika Jimbo la Igunga utarudiwa.

Huku akitoa mifano mbalimbali ya jinsi baadhi ya wanachama wa CCM walivyokuwa wakitoa rushwa, Dk Slaa alimtuhumu Mweka Hazina wa chama hicho, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi kwamba alikuwa kinara wa kutoa rushwa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga Oktoba mwaka uliopita.

“Chadema imejipanga kwa rufaa hiyo ya CCM ikiwa ni pamoja na kufungua kesi nyingine dhidi ya vigogo wa CCM, walioshiriki katika kampeni za uchaguzi huo,”alisema Dk Slaa.

Dk Slaa pia alimponda Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akieleza kuwa mdomo wake umemponza kwa sababu alikuwa akizungumza mambo ambayo hakujua madhara yake.

Wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali wa Mahakama Kuu alisema moja ya hoja saba zilizotolewa na Chadema ambayo mahakama iliikubali ni ile ya Mukama kudai Chadema kilipeleka makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga.

Dk Slaa alisema: “Mukama alikurupuka kwa kutamka maneno bila kufanya utafiti hali iliyosababisha CCM kupoteza jimbo.”

Alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa suala la CCM kuingiza silaha ndani ya nchi, bila kibali wala leseni na kuwapatia vijana wake mafunzo katika kambi za Ilemo, Iramba mkoani Singida linamhusu mwenyekiti wa chama hicho na siyo mtu mwingine.

Alidai kuwa wakati wa uchaguzi wa Igunga, vijana hao walikuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi akisisitiza kuwa suala hilo linamhusu mwenyekiti wa chama hicho akimtaka atoe majibu na ufafanuzi juu ya hilo.

Dk Slaa alisema kuwa siku ya jana ilikuwa ni kwa ajili ya wananchi wa Igunga kusherehekea na kupongezana kwa mshikamano waliouonyesha wakati wote wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, huku akitoa pongezi kwa mawakili waliosimamia kesi hiyo kwa kuiwakilisha vyema Chadema katika kesi hiyo.

Naye upande wake aliyekuwa mgombea wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Igunga Oktoba mwaka uliopita, Joseph Kashindye aliwashukuru wananchi walioiunga mkono Chadema akieleza kuwa wameonyesha ushirikiano mkubwa uliokipa ushindi chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kashindye aliwashukuru pia wananchi wa Igunga kwa kukichangia Chadema Sh6 milioni zilizosaidia kulipia gharama za kesi hiyo pamoja na malazi kwa mashahidi mbalimbali waliotoa ushahidi kwenye kesi dhidi ya CCM iliyotolewa hukumu wiki iliyopita kwa kutengua ushindi wa Dk Dalaly Kafumu wa CCM.

“Mahakama imetenda haki kwa kuwa imetoa hukumu ya haki…, nimeamini kuwa haki ya mtu haipotei. Awali nilidhani kuwa mahakama ni mali ya CCM kumbe si kweli,” alisema Kashindye na kushangiliwa na mamia ya watu waliofurika katika uwanja huo.

Kashindye aliponda ahadi zilizokuwa zikitolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwamba ndizo zilizofanya CCM kushindwa kesi.

“Watu wa ajabu sana, wametoa ahadi za kujenga madaraja, kusaidia chakula wakati hilo ni jukumu la Serikali,” alisema Kashindye akionyesha kushangaa.

Alibainisha kuwa wakati kesi hiyo ikinguruma mahakamani, alikuwa akitafutwa na wanachama wa CCM, lakini kutokana na kujua mbinu zao, aliamua kujichimbia kusikojulikana.

Dk Kafumu aliibuka mshindi katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana kuziba nafasi ya Rostam Aziz ambaye alijiuzulu kwa madai kwamba anaachana na siasa chafu ndani ya CCM.

Katika uchaguzi huo kulikuwa na upinzani mkubwa kati ya Dk Kafumu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye ambaye hakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo, hivyo kuamua kupinga matokeo hayo mahakamani. Kesi hiyo ilifunguliwa Machi 26, mwaka huu.
 
Source: Mwananchi

Thursday, August 23, 2012

Chenge kumtetea Mramba kesi ya ufisadi


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kesho itaanza kusikiliza utetezi wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. Bilioni 11.7, inayomkabili mawaziri wa zamani, Basil Mramba, Daniel Yona na Katibu mkuu wa Hazina, Gray Mgonja baada ya kukutwa wana kesi ya kujibu.

Utetezi huo utasikilizwa mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Jaji John Utamwa na Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu waliopewa kibali na Jaji Mkuu kuendelea kusikiliza kesi hiyo wakisaidiana na Saul Kinemela.

Upande wa Mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Osward Tibabyekomya akisaidiana na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kupambana na Kuzia Rushwa (Takukuru), Ben Linkolin.

Upande wa utetezi unawakilishwa na mawakili, Herbat Nyange, Cathbert Tenga na Elisa Msuya.
Mapema mahakama hapo bila kuacha shaka iliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili.

Awali mahakamani hiyo, upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya kuita mashahidi 13 na kuwasilisha vielelezo 26 mahakamani.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanadaiwa kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri na katibu mkuu walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

CHANZO: NIPASHE

Wednesday, August 22, 2012

Dovutwa amfananisha Lowassa na Kawawa

Mh Lowasa.
MWENYEKITI wa Chama cha United Peoples Democratic (UPDP), Fahmi Dovutwa, amemfananisha Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, marehemu Rashid Kawawa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Dovutwa alisema Lowassa hana tofauti na Kawawa, ambaye katika uhai wake akiwa waziri mkuu alibeba lawama za Serikali katika utawala wa awamu ya kwanza.

Dovutwa ambaye mwaka 2010 aligombea urais, alisema Lowassa hakuhusika katika kashfa ya rushwa iliyotokana na mkataba tata wa Richmond na kwamba alijiuzulu uwaziri mkuu ili kulinda heshima ya Serikali na si vinginevyo.

“Mwalimu Nyerere alipata kutoa hotuba siku moja akisema kwamba: ‘Namshukuru sana mzee Rashidi Mfaume Kawawa, amenisaidia sana.

‘Mambo yote ambayo amekuwa akilaumiwa Kawawa niliyafanya mimi na yeye (Kawawa) alibeba tuhuma hizo kwa ajili yangu’, haya ni maneno ya Baba wa Taifa na hotuba zake hizi zipo,” alisema Dovutwa akimnukuu Mwalimu.

Dovutwa aliongeza: “Kwa kauli hiyo ya Baba wa Taifa ni wazi Lowassa hakuhusika na kashfa ya Richmond. Kwa sababu maamuzi ya kiutendaji wa Serikali yako mikononi mwa Baraza la Mawaziri ambalo mwenyekiti wake ni Rais.

“Waziri yeyote hana uwezo wala mamlaka ya kuamua jambo bila ridhaa ya Rais. Lowassa aliwajibika ili kuilinda Serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete isianguke na kupisha uchaguzi mwingine,” alisema.

“Mwalimu Nyerere alielewa vizuri dhana ya uwajibikaji na Watanzania wengi hawakumwelewa Mwalimu Nyerere alipokuwa akiwarudisha baadhi ya watumishi ambao awali waliwajibika kwa tuhuma za kiutumishi.

“Kimsingi tuhuma alizokuwa amelaumiwa kiongozi mwandamizi wa Serikali zilikuwa ni tuhuma za kiongozi mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kufanya jambo au kulikataa.

“Ili kuilinda Serikali na kiongozi mkuu wa Serikali ndipo hutokea mtumishi mmoja wa Serikali kubeba lawama na tuhuma za wizara yake kwa manufaa ya Serikali yenyewe.

Hivyo dhana ya kuwajibika ilieleweka vizuri kwa Mwalimu Nyerere kuliko wasomi walio wengi wa ndani na nje ya CCM,” alisema Dovutwa.

Dovutwa alisema Lowassa ni kiongozi makini mwenye ujasiri ambaye aliweza kufanya mambo akiwa waziri mkuu, huku akiwatahadharisha wananchi kuwa makini na baadhi ya viongozi.

“Watanzania tusikumbuke kufanya mabadiliko ambayo huenda tukaondoa wala rushwa wadogo na kuingiza wala rushwa wakubwa zaidi,” alisema.

Dovutwa aliwataka Watanzania kutafakari juu ya mwenendo wa vyama vilivyoko bungeni, hasa kutokana na Bunge kuchafuka kutokana na kashfa ya rushwa inayowahusisha wabunge.


Source:www.jamiiforum.com