Pages

Sunday, January 27, 2013

TAARIFA YA NDUGU ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA


Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara

Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.

Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.

Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.

Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara na hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.

Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro
huu.

Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.

Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.

Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.

Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.

Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili.

Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (zittokabwe.com).

Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la Mtwara.

Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.

Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.


Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara

Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.

Tufanyeje?

Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
  1. Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.
  1. Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
  1. Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.

Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa chama kutoa ridhaa.


ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Kaskazini (Chadema)
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni

Saturday, January 26, 2013

Taswira vurugu za jana Mtwara

Mahakama ya mwanzo iliyochomwa moto

                                                         Mwandishi wa Chanel 10 aliyepigwa jiwe
Kijana akishikiliwa na Askari baada ya kukamatwa

                                                     Chini ya ulinzi

                                                  Nyumbani kwa Mh. Hawa Ghasia hakukusalimika

Source: Jamii Forum

Friday, January 25, 2013

Mkuu wa kaya ilipo gesi anusurika kutekwa, wananchi wachoma moto gari

Mabaki ya gari lililochomwa
MKUU wa Kaya ya Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa mkoani Mtwara, Bibi Somoe Mtiti (106) amenusurika ‘kutekwa’ na mtu anayeaminika na wakazi wa eneo hilo kuwa ni mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa baada ya wananchi kuvamia gari lake na kuliteketeza kwa moto jana usiku.

Hivi karibuni Bibi Mtiti aliionya Serikali juu ya mpango wake wa kusafirisha gesi ghafi kwenda Dar es Salaam kwa madai iwapo itapuuza onyo hilo bomba hilo litasafirisha maji badala ya gesi iliyokusudiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa mhusika hajakwenda polisi kulalamika.

Kwa mujibu wa wanakijiji hao, mtu huyo ambaye ana asili ya kijiji hicho waliyemtambua (jina linahifadhiwa) aliwasili kijijini hapo jana saa 10 jioni akiwa na gari dogo aina ya Mark II na kwenda nyumbani kwa shangazi yake.

Habari zinadai kuwa saa 2 usiku mshukiwa huyo alidaiwa kwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti akiwa na gari pamoja na shangazi yake.“Unajua yule bibi tunamlinda, sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu wakaanza kujiuliza linafanya nini…wakaanza kusogea, kadiri muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo watu walivyozidi kuongezeka,”alisema Juma Ayoub mkazi wa kijiji hicho.

Asha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi Mtiti, akihadithia juu ya tukio hilo, alisema yapata saa 2 usiku wakiwa wanakula chakula walipokea wageni wawili ambao baada ya kumaliza kula waliomba kuongea na mkuu huyo wa kaya.

“Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na bibi…alimuuliza bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu hawezi…wakaniuliza mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia siwezi…akasema ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia...wamjie bibi wakazungumze naye mambo ya gesi,” alisema Hamis.

Aliongeza kuwa “Kama bibi yupo tayari Jumanne ijayo watamfuata kwa gari…mimi nikasema sitaki…nilipochungulia nje nikaona watu wengi wamezunguka.”

Kwa upande wa mtoto mwingine wa bibi huyo alisema,” Kwa kuwa tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia haufai, akawa anabisha, tukaendelea kumsihi..wakati huo watu wanazidi kuongezeka…alipotoka akakosea njia, alipopita hakukuwa na njia…watu walimfuata wakaanza kumrushia mawe…aliacha gari akakimbia…ndipo wananchi walipoliteketeza gari kwa moto,” alisema Manzi Mohamedi Faki mtoto wa tano wa Bibi Mtiti.

Shangazi wa mtuhumiwa amethibitisha kumpokea mwanaye huyo na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimwomba mkuu huyo wa kaya akubali kuondoka naye kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ametumwa na viongozi wake wa juu.

“Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu pale, naye alikimbia na ndipo walipochoma moto gari,” alisema shangazi huyo.Alifafanua kuwa “Huyu mwanangu anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi Usalama wa Taifa…nadhani alirudi jana hiyohiyo Mtwara.”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Tostao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ofisi yake haikupokea mgeni yeyote kutoka serikalini kwa siku hiyo. “Ni kweli gari limechomwa lenye namba za usajili T 609 BXG mali ya Mussa Babu…taarifa hii ni kwa mujibu wa nyaraka tulizookota kutoka ndani ya gari hilo,” alisema Tostao.
 
Selemani Babu alikanusha madai ya yeye kwenda kijijini hapo jana na alisema, “Hapana, hapana labda umekosea…na..na..na..umekosea…sijakwenda Msimbati jana…kwa nini asiwe Mussa, umekosea siyo mimi kwa heri.”
 
Source: Mwananchi

Thursday, January 24, 2013

Moto wa gesi wavuka nje ya mipaka

 
BALOZI wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik ameonya kuhusu hatari za kugeuza suala la gesi ya Mtwara kuwa mtaji wa kisiasa.

Wakati Norway ikisema hayo, Mkurugenzi wa Uchumi katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Nyamajeje Weggoro amesema mgogoro huo utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano yaliyojaa lugha na kauli laini isiyo na vitisho wala kuwabeza wananchi.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na mijadala, mizozo na maoni kutoka kwa kada mbalimbali kuhusiana na suala la gesi hiyo inayopatikana katika eneo la Msimbati, Mtwara.

Akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa, Lushoto mkoani Tanga, Balozi Klepsvik alisisitiza kuhusu haja ya Watanzania kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya kuangalia masilahi ya watu binafsi au taasisi.

“Norway ilipogundua nishati ya petroli tulikubaliana kitu kimoja kwamba suala hili lisihusishwe na kampeni za kisiasa. Hii itasaidia kuweka mbali masuala ya rasilimali na siasa,” alisema.

Balozi huyo alisema gesi ya Mtwara inapaswa kuwanufaisha wananchi wa Mtwara kwanza kabla ya watu wengine, lakini masilahi ya taifa lazima yawekwe mbele katika mjadala wa suala hilo.

Klepsvik alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika masuala muhimu ya maendeleo na kueleza kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kwa kuwahusisha watu wa kada zote hasa wanawake.

Hata hivyo, alisema endapo mambo yatafanyika kwa utaratibu wake, gesi iliyovumbuliwa inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yao.

“Tulipogundua gesi na petroli, hatukuwa tunafahamu lolote, tuliita wageni wakatufanyia kazi ya kuchimba, wakati huo tulipeleka watu wetu vyuo vya nje kusoma na baada ya miaka 10 sasa tunashughulika wenyewe na kila kitu kwa manufaa ya taifa zima,” alisema Klepsvik.

EAC yashauri mazungumzo
Akizungumzia mgogoro huo, Dk Weggoro alisema umetokana na wananchi kutopata elimu ya kutosha kuhusu namna watakavyofaidika na rasilimali hiyo inayopatikana katika eneo lao.

“Mgogoro wa gesi Mtwara utamalizika kwa njia ya mazungumzo na majadiliano lakini siyo vitisho,” alisema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya EAC jana.

Alisema haamini kama ni kweli wananchi wa Mtwara hawataki Watanzania wenzao wafaidike na gesi inayopatikana mkoani humo, bali wanahofia hatima ya maisha, faida na masilahi yao kutokana na rasilimali hiyo.

“Viongozi lazima wazungumze, wajadiliane na kufikia mwafaka na wananchi (wanaMtwara), kuhusu mambo yanayogusa maisha na masilahi yao. Ni vyema watu ambao maliasili na rasilimali zinapatikana katika maeneo yao wanufaike kwanza kabla ya wengine.”
 
Soma zaidi.....Mwananchi

Tuesday, January 22, 2013

Vigogo Bandari wafukuzwa kazi

Waziri wa uchukuzi Dr Harison Mwakyembe amewatimua kazi vigogo watano wa mamlaka ya bandari Tanzania (TPA), baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka , ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Soma zaidi....Habari leo

Wednesday, January 16, 2013

Mbatia: Umbea umechochea yaliyomkuta


 
MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema yaliyomkuta kwenye yake ziara mkoani Mtwara ambako amelazimika kuikatisha, yametokana na umbea aliouita ni wa mwaka 2013.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, alisema hayo jana kwenye Ofisi za Bunge Dar es Salaam.

“Unasemaje (anamuuliza mwandishi), ngoja nikwambie kilichotokea kimetokana na umbea tu wa mwaka mpya 2013, wewe tambua hivyo na sitazungumza lingine zaidi,” alijibu kwa kifupi akionyesha kukwepa kulizungumzia suala hilo zaidi.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini viliripoti kuhusu Mbatia akiwa na wabunge wa chama chake, Moses Machali (Kasulu Mjini ) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) walilazimika kujifungia ndani ya ofisi za NCCR- Mageuzi wilayani Mtwara Mjini.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya baadhi ya wananchi kuamua kumrushia chupa tupu za maji, huku wakimfuata kabla ya kuizingira ofisi hiyo wakiimba nyimbo za kumshtumu kuwa ni mamluki.

Ilielezwa kuwa, hali ilikuwa tete eneo la ofisi hiyo hasa baada ya giza kuingia, kwani wananchi walianza kurusha mawe juu ya ofisi hiyo na wengine kujaribu kuvunja mlango na kurusha vitu vinavyodiwa kuwa ni baruti zinazotumika kuvulia samaki .

Hali hiyo ilisababisha polisi waliofika kumuokoa kutumia mabomu ya machozi.
Mapema mwaka huu baadhi ya wananchi wa Mtwara waliandamana wakipinga gesi kusafirishwa kuletwa Dar es Salaam.
Badala yake, walitaka mtambo wa kuzalisha umeme kujengwa mkoani humo.

Source: Mwananchi

Tuesday, January 15, 2013

Unyama mkubwa Mbeya, wawili wazikwa hai

WAKAZI wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Watu hao, Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, walizikwa wakiwa hai pamoja na aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, marehemu Nongwa Hussein.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa tano na sita mchana, muda mfupi kabla ya maziko ya Hussein.

Kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu, Molela na Nachela kwa nyakati tofauti walipigwa hadi kuzirai na watu wanaodaiwa kushiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hussein.

Silwimba alisema Hussein alifariki dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini inaonekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa huo ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jana mchana, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Momba aliyefahamika kwa jina la Wendo aliongoza operesheni ya kufukua kaburi walimozikwa watu hao, ambao walikutwa wakiwa wameshafariki dunia.

Silwimba alisema miili ya Molela na Nachela ilifanyiwa uchunguzi, kisha kukabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao ambao waliifanyia mazishi jana mchana.

Mkasa wenyewe
Kundi la vijana tisa ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakichimba kaburi la marehemu Hussein walianza msako katika Kijiji cha Karungu wakiwatafuta wale waliowatuhumu kwamba ni wachawi na kwamba walihusika na kifo chake.

Silwimba alisema katika harakati zao, walikwenda nyumbani kwa George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu lakini hawakumkuta, hivyo kuamua kuchoma moto nyumba yake kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho.

“Baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda hadi nyumbani kwa Mzee Molela kisha wakamkamata na kumpiga sana hadi hali yake ikawa mbaya kisha wakambeba hadi eneo la maziko,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea kwenye msiba walimkuta Mama Nachela naye wakamkamata na kuanza kumpiga hadi akazimia na yeye pamoja na Molela waliwavuta hadi kwenye kaburi ambako mazishi ya Nongwa (Hussein) yalifanyika.”

Alisema baada ya jeneza kushushwa kaburini, vijana hao wanaodaiwa kwamba walikuwa na hasira walimvuta Molela na kumwamuru kuweka udongo kaburini, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya kushindwa walimsukumiza kaburini na baadaye walimvuta yule mama (Nachela) ambaye naye alikuwa hajitambui na kumtupa ndani ya kaburi halafu wakawafukia wote, kisha wakaondoka,” alisema Kaimu Ofisa Mtendaji huyo.
 
Alisema mwingine aliyekuwa akisakwa na vijana hao ni Fotino Sichilongwa na kwamba kabla ya kufanya vitendo hivyo, vijana hao walimkamata Mwenyekiti wa Kitongoji, Alfred Kukwe na kumfunga miguu na mikono kwa kutumia kamba, wakamlaza kifudifudi, kisha kumnyang’anya simu yake ya kiganjani ili asiweze kutoa taarifa kokote.
Alisema Kukwe alifunguliwa kamba hizo saa saba na nusu mchana na ndipo alipopiga simu sehemu mbalimbali kutoa taarifa za tukio hilo.

Silwimba alisema baada ya taarifa hizo kusambaa kijijini Karungu, mwenyekiti wa kijiji hicho na ofisa mtendaji wake, walikimbia na kwenda kujificha kusikojulikana wakihofia kudhuriwa na vijana hao.

“Polisi walipofika jana (juzi) jioni walikuta vijana wote waliohusika wamekimbia na hawajulikani walipo maana nyumba zao zimefungwa, hili ni tatizo kubwa maana limesababisha taharuki kubwa hapa kijijini,” alisema.

Wawili mbaroni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kulikuwa na taarifa kuwa Molela na Nachela wana undugu. Hata hivyo, habari kutoka kijijini Karungu zimesema hawana undugu wowote.

Kamanda Diwani ambaye aliwashutumu wananchi kwa kujichukulia sheria mkononi, alisema hadi sasa watu wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.“Tunawashikilia watu wawili ambao tunaamini walikuwa vinara wa tukio hili la mauaji,” alisema Diwani.
Kamanda huyo aliitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake waheshimu na kutii sheria bila shuruti na kuachana na imani za kishirikina.

“Kila mmoja afanye mambo yake kwa kujiamini. Hii ya kuendekeza imani za kishirikina ina madhara na zaidi ni kurudisha nyuma maendeleo. Jamii inatakiwa kutafuta njia halali kufikisha kero na malalamiko badala ya kutumia vurugu na fujo na kusababisha mauaji.”
 
Source: Mwananchi