Pages

Tuesday, July 3, 2012

Freemasons Ni Abrakadabra


Na Maggid Mjengwa,

MWANDISHI Mtanzania, Profesa Euphrase Kezilahabi, anaandika juu ya bwana aliyefika kwenye ngoma asiyoijua. Akashtuka alipowaona wapiga ngoma, akauliza;

“ Nyinyi ni nani?”

“ Sisi ni wapiga ngoma”, mmoja kati yao akamjibu.

” Kwa nini mpo mahali ambapo hamtegemewi kuwa?”

” Hapa ni wapi?” Wapiga ngoma walimwuliza bwana yule. Naye akajibu;

” Kama ningejua nisingekuwa hapa kuonyesha siri ya ufundi wangu! Na hiyo ngoma yenu inaitwaje?”

” Tutajua Manju Mkuu atakaposimama katika kitovu cha duara”, mmoja wao alijibu.

” Hivi sasa tunajifunza wimbo wetu wa kwanza.”

” Na wachezaji wako wapi?”, aliuliza bwana yule.

” Yeyote yule anayeweza kufikiri”. Mwingine alijibu: “Lakini wale wachezao vizuri ni wale wanaovuka mpaka huo na kuingia katika ulimwengu huru. Hao hatunao wengi. Tulio nao wengi ni wanafiki wanaojidai kujua. Wanatufaa, maana tunawatumia kama wachekeshaji”. (Rejea Prof. Euphrase Kezilahabi, Nagona, uk.39)

Naam, maandiko hayo ya Profesa Kezilahabi yamenivutia kuendelezea makala haya niliyoanza nayo juma la jana. Maana, ni maandiko yenye kutuma ujumbe wenye maana kubwa kwetu.

Baadhi ya wasomaji wangu wamenitaka nifafanue zaidi kuhusu hili la Freemasons, na kuna waliotaka kujua maana ya neno ‘abrakadabra’.

Hakika, kama anavyoandika Profesa Kezilahabi, nawaona Watanzania wengi leo tunacheza ngoma tusioijua. Na baadhi yetu; hususan wanahabari, wanacheza vibaya zaidi, maana, hawajavuka mpaka na kuingia katika ulimwengu huru.

Ndio hawa, kila kukicha, wanaeneza uzushi na uvumi wa hili na lile. Jamii bado ina imani na wanahabari, hivyo, haraka sana wanahabari huchangia kuipotosha jamii.

Hili la Freemasons ni moja ya upotoshaji huo. Sasa limefanywa kuwa ni ’abrakadabra’. Mwandishi yeyote makini, akikaa chini na kusoma vitabuni na hata mtandaoni juu ya habari za Freemasons, basi, hawezi kuja na simulizi za ajabu ajabu juu ya Freemasons kama tunazozishuhudia sasa katika jamii yetu.

Kimsingi, Freemasons tunayoisoma vitabuni imekuwepo tangu karne ya 14. Ni jumuiya ambayo wanachama wake wapya huingia kwa kutambulishwa na wanachama waliopo. Iko katika nchi nyingi duniani. Imejengeka katika misingi ya imani ya Kikristo, na inatokana na kundi la wajenzi katika jamii wa tangu karne ya 14.

Tunasoma, kuwa enzi hizo, wajenzi hao wa majengo hawakutaka kumilikiwa na wenye kujenga majengo yao. Walikuwa wakijenga, na wakimaliza wanakwenda kujenga mahali pengine walipotaka. Na waliweza pia kukatisha kujenga kama hawakupatana na mwenye jengo. Ndio asili ya kuitwa Freemasons ambayo ina tafsiri ya Wajenzi Huru .

Na enzi hizo kando ya sehemu ya ujenzi lilijengwa banda la wajenzi. Ikawa kama karakana yao. Banda hilo lilijulikana kama lodge. Ni neno ambalo linatumika hadi hii leo ikiwa na maana ya sehemu ya wageni kukaa kwa malipo.

Freemasons, kama jumuiya, imekua na hata ikawa si ya Wajenzi Huru tu; bali jumuiya yenye taratibu zake ambazo imewaingiza hata wasio wajenzi, bali watu wa kada nyingine walioingia humo. Ni pamoja na wafanyabishara.

Hivyo basi, Freemasons haikuanza leo, na taarifa zake ziko vitabuni na hata mitandaoni. Bahati mbaya kwa nchi yetu abrakadabra imeingizwa katika simulizi ya hao Freemasons kiasi cha jamii kuaminishwa kuwa ni kitu cha ajabu sana. Kwamba ni imani ya kishetani na inahusishwa na utajiri wa haraka.

Na sisi Watanzania ni watu wa ajabu pia. Tujiulize; hivi kama hiyo Freemasons ingekuwa ni mahali pa kuingia na kujipatia utajiri wa haraka, si tungeona watu wa dunia hii wakipanga foleni ndefu kujiunga na mtandao huo? Kwani katika dunia hii masikini wako Tanzania tu?

Tunasahau kuwa, katika dunia hii kuna masikini wengi na wenye elimu pia. Wakati masikini wenzetu wanavyopambana kwa kutumia elimu yao kujikomboa kutoka kwenye umasikini wao, sisi tumekalia kuimba na kucheza ‘ngoma tusiyoijua’. Kila kukicha Freemasons, Freemasons!

Na wengine tungeamua kuwa watu wa hovyo hovyo tungejipatia fedha za bure tu. Maana, kwa kuandika habari za Freemasons juma la jana , basi, nimepokea simu nyingi za watu wenye kutaka kujiunga na mtandao huo kupitia kwangu!

Kwamba wako tayari kunitumia malipo ya uanachama! Niliwajibu kuwa mimi si mwanachama wa Freemasons, na kwamba nimeandika tu, na nikawaambia kuwa wanavyozidi kunipigia simu wanazidisha umasikini wao, maana wanatumia fedha zao.

Naam, Bwana Yesu alipotembelea Mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, miongoni mwao alikuwa Simoni. Yesu akasema:"Simoni, acha kuvua samaki, enenda ukavue watu."

Hakika, na watu wetu wamezama kwenye mambo ya abrakadabra. Wanahitaji maarifa ya kuwatoa hapo walipo. Wanahitaji elimu pia. Maana, mengi ya tunayoyashuhudia sasa ni abrakadabra.

Neno abrakadabra humaanisha kuwa ni mambo ya hila na ghilba. Ni neno la ‘kimazingaombwe’. Maana, dunia hii mazingaombwe yapo, ni sanaa. Anayekutamkia abrakadabra au ndumba nangae hana cha maana alichokutamkia bali anaichota akili yako kimazingaombwe. Anakudanganya.

Na wanaodanganywa ni Watanzania waliojifunika au kufunikwa vilemba vya ujinga! Na wanaojitokeza sasa ni ‘manabii wa siku za mwisho’. Wanatujenga hofu. Nao wanatajirika kwa hofu na ujinga wetu.

"Simoni, acha kuvua samaki, enenda ukavue watu."

Ndio, samaki wako huru majini, lakini kuna wanadamu wengi walio bado kwenye utumwa wa fikra. Bado wanaogelea kwenye povu la ujinga. Wako gizani kwenye nuru inayoangaza mchana. Wanahitaji kuvuliwa kutoka dimbwi la ujinga.

Mwanafalsafa, John Rawls, anasema: “Hata kama utakalo ni haki yako ya asili, lakini kama hilo utakalo halina faida kwa walio wengi, basi, si haki yako kulifanya. Hakika, wale wenye kusambaza uvumi na uzushi wa hili na lile katika jamii wanapaswa kukemewa na hata kulaaniwa.

Maan; hata kama ni haki yao kujitafutia riziki, lakini kwa vile kusambaza uzushi na uvumi ni mambo yasiyo na faida kwa walio wengi, basi, si haki yao kuyafanya hayo. Hivyo basi, tuangalie hata taratibu za kisheria za kuwashughulikia watu hawa. Mjadala huu utaendelea.

No comments:

Post a Comment