SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete
kusema daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa
mshahara wa Sh3.5 milioni aache kazi, viongozi wa dini, wanasiasa, wabunge na
wasomi wamemtaka apunguze jazba.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema
mgogoro wa madaktari na Serikali bado unajadilika huku Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika akienda mbali zaidi na kusema Serikali iache kisingizio
cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro baina yake na madaktari, wakati
yenyewe inajadili na kutoa maelezo.
Juzi, katika hotuba yake ya kila mwisho wa
mwezi, Rais Kikwete alisema Serikali haiwezi kuahidi kuwa inao uwezo wa
kuwalipa madaktari mshahara huo na posho zote kwani ikifanya hivyo malipo ya
daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi kitu ambacho
hakiwezekani.
Jana, wakizungumza kwa nyakati tofauti,
wadau hao walisema mgogoro huo kati ya Serikali na madaktari bado unajadilika
na kusisitiza kuwa hotuba ya Rais Kikwete haijajibu madai ya madaktari.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Bashiru Ally alisema ingekuwa jambo jema kama kungekuwa na uwezekano wa
mazungumzo kuendelea.
Alisema kauli ya Rais ni upande wa
Serikali hivyo, ingekuwa vyema kama madaktari nao wangepata nafasi ya
kujieleza.
Wanasiasa
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi),
Moses Machali alimtaka Rais apunguze hasira na kuitaka Serikali ikubali kurudi
katika meza ya mazungumzo hata kama ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwapeleka
mahakamani madaktari waliogoma.
Alisema kama Serikali haiwezi kulipa
kiwango cha mshahara kilichopendekezwa na madaktari, irudi katika meza ya
mazungumzo ili kutafuta suluhu ya mgomo huo unaowaumiza zaidi wananchi.
“Warudi kwenye meza ya majadiliano siyo
kila mmoja kusema la kwake na kuacha mgomo kuendelea huku, watu wakiteseka
hospitalini bila msaada wowote,’’ alisema Machali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi
(CUF), Julius Mtatiro alisema Serikali haipaswi kuwafukuza madaktari kwa kuwa
imetumia gharama kubwa kuwasomesha.
“Ikiwafukuza madaktari italazimika
kuwaleta walio nje ya nchi ambao ni gharama kubwa… Serikali itatue mgogoro
huu,” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
alisema Serikali iache kutumia kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili
mgogoro wa madaktari wakati yenyewe ikitoa ufafanuzi.
“Uamuzi wa Serikali kutoa kauli kupitia
hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge kujadili hotuba husika ambayo
awali, ilielezwa kuwa ingetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni.
Inawanyima haki wabunge wasitimize wajibu wa kikatiba wa Ibara 63 (2) wa
kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema, kwa kuwa Bunge litajadili
mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012
na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia leo, ni
muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na
kutimiza wajibu wa kikatiba.
“Hotuba ya Rais imeendeleza kauli za
upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali kuhusu mgogoro huo bila
taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielelezo vya upande wa pili, hivyo
Serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani.
Viongozi
wa dini
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC)
Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo alisema madaktari hao wanatakiwa kurudi kazini
kwa kuwa tayari Serikali imeshasema kuwa haina fedha za kuwalipa na kuongeza
kuwa hata kama wana madai yao, wadai wakiwa kazini.
“Asilimia kubwa ya madaktari wamesomeshwa
na Serikali… Serikali hiyohiyo inawaeleza kuwa haina fedha za kuwalipa kama
wanavyotaka, binafsi nawaomba tu warudi kazini kwa kuwa mgomo wao unawaathiri
zaidi wananchi kuliko hata hao viongozi wa Serikali.
“Tunajua tulikotoka ila hatujui
tunakokwenda, kama ni kuboreshwa kwa sekta nzima ya afya, Serikali imesema
itatekeleza hilo, haiwezi kuyatekeleza kwa siku moja, haya mambo yanajadilika.
Alisema kama Serikali itakuwa na makosa
yake, itayajibu mbele za Mungu... “Madaktari watekeleze wajibu wa kazi yao kwa
uwezo wa Serikali iliyopo madarakani.”
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la
Kagera, Dk Methodius Kilaini alisema kanisa hilo haliwezi kuunga mkono mgomo
huo.
Alisema pamoja na kuwa madaktari wana
madai yao, jukumu lao kubwa ni kufuata maadili ya kazi yao ambayo hayawaruhusu
kugoma.
Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania, Askofu David Mwasota alisema madaktari wanatakiwa kutenganisha siasa
na maadili ya kazi yao.
“Hata kama Serikali ina makosa yake
lakini, wao kuendelea kugoma si jambo zuri kwa jamii na hata mbele za Mungu,
watumie njia nyingine kudai madai yao, lakini waendelee kutoa huduma. Madaktari
ni watu muhimu, kurudisha viungo vya binadamu katika hali ya kawaida si kazi
ndogo, warudi kazini kuokoa mamia ya Watanzania maskini.”
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu wa
Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha Abdulkarim Jonjo alisema ipo haja kwa
Serikali kukaa meza moja na madaktari hao.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mjini Kati, Thomas Laizer alisema mgogoro
wa madaktari umalizwe kwa mazungumzo.
Alisema Serikali inapaswa kuwa wazi
inapozungumza na madaktari kwa kueleza ni mambo gani yanawezekana na kwa muda
gani ili, kuondoa migogoro.
Akizungumza juzi katika ibada maalumu
katika kanisa la KKKT Kimandolu, alisema ili kuondoa hisia kuwa Serikali
inahusika na tukio la kutekwa Dk Ulimboka ni lazima iundwe tume huru.
“Nadhani ili kuondoa haya maneno ambayo si
jambo dogo, Serikali inapaswa kuunda tume huru kuchunguza tukio hili, kwani
inawezekana waliohusika ni watu wengine tu wenye nia mbaya na Serikali lakini
ili ukweli ujulikane ni muhimu kuwepo tume huru,” alisema Askofu Laizer.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj
Mussa Salum aliwataka madaktari kutii agizo lililotolewa na Mahakama kwa kurudi
kazini.
“Rais ameshaeleza wazi kwamba Serikali
haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, warudi tu kazini na kuweka masilahi
ya Watanzania mbele na kuacha kutanguliza masilahi binafsi,” alisema Sheikh
Salum.
Wanaharakati
Mkurungezi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hotuba hiyo ya Rais
haina jipya zaidi ya kurudia maelezo yake ya awali alipokutana na Wazee wa Mkoa
wa Dar es Salaam.
“Nilitarajia kuwa hotuba itakuwa tofauti
lakini sivyo. Amerudia maelezo yaleyale aliyoyasema Machi 12 (mwaka huu)
alipokutana na wazee katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,” alisema Bisimba.
Wakili Peter Jonathan alisema kama kweli
Serikali inataka kurudisha imani kwa Watanzania kuhusu tukio la Dk Ulimboka ni
lazima ijisafishe kwa kuunda tume huru nje ya Serikali.
“Watafute hata Jaji mstaafu, si lazima
atoke Tanzania kuongoza tume huru ikibidi tuchukue hata nje ya nchi ili wakitoa
taarifa iweze kuaminiwa na jamii na hiyo ndiyo dhana sahihi ya utawala bora,”
alisema.
Mjumbe wa Chama cha Watabibu wa Tiba Asili
(ATME), Boniventure Mwalongo ameitaka Serikali kuacha kutumia nguvu
kushughulikia madai ya madaktari badala yake ipanue wigo wa majadiliano ili
kutatua tatizo hilo.
“Nimesikiliza hotuba ya Rais lakini,
haijaonyesha kama kuna jawabu la mgomo hivyo wapanue wigo wa majadiliano ili
kumaliza mgogoro huu,” alisema Mwalongo.
Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe,
Nora Damian, Bakari Kiango, Freddy Azzah,
Daniel Mwingira, Dar; Daniel Mjema, Moshi; Mussa Juma, Arusha na Frederick
Katulanda, Mwanza.
Chanzo:
http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment