"NI saa 12:45 asubuhi, bado
kiza kimetanda katika eneo hili la Msitu wa Mabwepande. Mbele yangu namwona mtu
akiwa amekaa chini, pembeni ya barabara akiwa amelowa damu mwili mzima.
"Ninapomkaribia nasikia
sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani… naomba msaada
jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza Abdallah, mtu wa kwanza
kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka baada
ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam.
Abdallah, anasema mara baada
kumwona daktari huyo akiwa katika hali hiyo, alijaribu kumkokota kumtoa eneo
hilo, lakini alishindwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.
Baada ya hapo, aliamua kusubiri
mtu mwingine apite eneo hilo ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi
Bunju.
Anasema muda mfupi baadaye aliona
gari likija mbele yao, akalinyooshea mkono kulisimamisha. Liliposimama,
akamweleza dereva hali aliyokuwa nayo Dk Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa
haraka.
Abdallah ambaye hadi wakati huo
alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia kuwa ni kiongozi wa madaktari
kutokana na sura yake kuvimba, anasema walimwingiza katika gari hilo na
kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi Bunju.
Anasema, Dk Ulimboka wakati huo
alikuwa akiendelea kuvuja damu katika baadhi ya majeraha yake huku akiwa hana
suruali na kubaki na bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.
Kituo cha Polisi Bunju
Baada ya kumfikisha kituoni hapo,
walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha hapo.
Polisi baada kumhoji Dk Ulimboka,
aliwatajia namba ya simu ya rafiki yake aitwaye Dk Deo. Walipompigia na
kumweleza tatizo hilo, aliamua moja kwa moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, kutoa taarifa hizo na hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo
akiwamo Mkurugenzi wake, Hellen-Kijo Bisimba.
Wawasili kituoni
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu Tanzania wa kituo hicho, Onesmo Olengurumwa, anasema
waliwafika Polisi Bunju saa 3:36 asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa
amekalishwa kwenye benchi huku damu ikiwa imeganda kwenye majeraha mwilini.
Olengurumwa anasema waliwahoji
polisi waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia kiasi hicho muda
mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili kuwahi kupatiwa matibabu.
Olengurumwa anasema polisi
walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike
Baada ya muda mfupi, akiwa
ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali, Dk Ulimboka aliomba maji ya kunywa
akisema ana kiu sana, lakini alipopewa, alikunywa kidogo akashindwa.
Anasema wakiwa njiani, alikuwa
akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa tukio la
kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua.
"Jamani hawa watu walitaka
kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara akisema Dk
Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.
Maelezo ya Dk Ulimboka
Baada ya Dk Ulimboka kuokotwa
aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada ya kutolewa msituni na
mazungumzo yake yalikuwa hivi;
“Nilikamatwa na watu hao usiku wa
Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club, Kinondoni na daktari mwenzangu baada ya
kupigiwa simu na mtu mmoja ambaye alidai kuwa anafanya kazi Ikulu.
“Kuna jamaa mmoja anafanya kazi
Ikulu, kama siku tatu mfululizo alikuwa akitaka kukutana na mimi ila
nilishindwa kukutana naye kwa kuwa nilikuwa na kazi nyingi na wakati mwingine
mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.
Huku akizungumza kwa taabu
kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena simu
na kumtaka wakutane.
“ Jana (Jumanne) alinipigia simu
na nikamwambia daktari mwenzangu twende tukaonane naye, wakati huo alitueleza
kuwa alikuwa maeneo ya Kinondoni Stereo,” alisema Ulimboka na kuongeza:
“Tulipofika maeneo hayo
tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye tukamweleza sehemu
tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”
Alisema kuwa, wakati anakutana na
mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.
“Kwa kweli siku ile nilivyoonana
na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa wakati wakiendelea
na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu yule.
“Katikati ya maongezi nikaona
ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka kuagana alikuwa akizungumza na simu,
sijui nini kilikuwa kinachelewesha sisi kuagana,” alisema Dk Ulimboka na
kuongeza:
“ Ghafla walitokea watu kama
watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa
mimi.
Wakati sijakaa sawa, waliniburuza
hadi barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”
Aliongeza, “Nilipowauliza
wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi nasumbua sana na nitajua hukohuko,
waliniingiza katika gari jeusi, lakini halikuwa na namba. Niliwauliza kosa gani
nimefanya? Hawakunijibu kitu na kusema, we twende utajua hukohuko.’
Alisema alipokuwa ndani ya gari
hilo watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya Victoria, walichukua
sweta nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya ashindwe kuona
kinachoendelea ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.
“Walinipiga mateke ya mbavuni,
wakati mwingine walitumia vitako vya bunduki, kila nilipokuwa najaribu
kuangalia ninapokwenda nilishindwa,” alisimulia Dk Ulimboka.
Alisema kuwa watu hao walimpeleka
katika nyumba moja ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha na kuanza
kumshambulia kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati huo, wote
walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.
“Tangu saa sita usiku mpaka saa
9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu, kuna wakati nilijaribu kukimbia wakapiga risasi
juu nikasimama na sikuweza kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“Nilisimama, wakaendelea
kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome sindano ya sumu nife au
kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa meno na kucha kwa kolea huku
wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari."
Alisema kuwa, watu hao walikuwa
na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.
“Waliniambia kuwa ninajua
ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma sindano ya sumu nife au wanikanyage na
gari nife,” alisimulia.
Dk Ulimboka alisema kuwa awali
hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa alidhani ni polisi, lakini baadaye
alishindwa kuwaelewa kwani watu hao walimchanganya.
“Sikuweza kuwatambua ila naweza
kusema ni askari, walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi na
wakati huo nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama maeneo ya Mwenge hivi,”
alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa baadaye alipoteza
fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao kwa mbali.
“Nilikuwa sioni na nilipoteza
fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari lilitembea muda mrefu, sikujua ni
wapi tunakwenda, kumbe ndio huko Mabwepande,” alisema.
Alisema kuwa walifika maeneo ya
barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.
“Waliniburuza na kuniacha huko na
muda wa saa kumi alfajiri ndipo nikazinduka na kuanza kujiburuza kuelekea
barabarani ambako nilisaidiwa na mtu mmoja ambaye simtambui,” alisema Dk
Ulimboka.
No comments:
Post a Comment