Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili ilikutana tarehe 28 Juni 2012 kujadili na kutathmini hali ya
utendaji na utoaji wa huduma hivi sasa katika Hospitali. Imebainika kwamba
utoaji huduma umeathirika kutokana na mgomo wa baadhi ya madaktari unaondelea
kwa takriban wiki moja sasa tangu ulipoanza Jumamosi ya tarehe 23 Juni 2012.
Baada ya tathmini hiyo, Bodi ya Wadhamini imeagiza yafuatayo:(i) Madaktari
waliopo kazini waendelee na kazi kama kawaida;(ii) Madaktari waliogoma warejee
kazini kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na.
76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.(iii)
Madaktari waliopo likizo warejee kazini mara moja. Utaratibu wa kufidia likizo
na nauli zao umeandaliwa. (iv) Uongozi wa Hospitali uwachukulie hatua za
kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi
bila sababu za msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za kazi;(v)
Uongozi wa Hospitali ufute mara moja ‘rotations’ za Madaktari waliopo kwenye
mafunzo kwa vitendo (interns); na(vi) Uongozi wa Hospitali uwapange (re-deploy)
Madaktari na Madaktari Bingwa waliopo kwenye maeneo yaliyoathirika wakati huu
wa mgomo
Aidha, Bodi ya Wadhamini
inawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote ambao wameendelea kuwahudumia
wagonjwa wetu na wananchi kwa ujumla. Vilevile, Bodi ya Wadhamini inawasihi
madaktari na wafanyakazi wote wawe na subira na waheshimu sheria, kanuni na
taratibu zilizopo pamoja na maadili ya taaluma zao.
_________________
Dkt. Gabriel Upunda
KAIMU MWENYEKITI BODI YA WADHAMINI
(source: www.mjengwa.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment