" Elimu ndio ufunguo wa maisha" hii ni kauli maarufu na kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa elimu katika maisha. Elimu kwa maana isiyo rasmi ni mchakato wa kuelimisha ama kuelimishwa jambo usilolijua ili uweze kupata ufahamu chanya ama hasi wa jambo hilo.
Ni miaka mingi imepita tangu nianze kusikia matatizo ya walimu na serikali, kikubwa walimu wakilalamikia maslahi duni wanayopata huku serikali ikjigamba kutatua matatizo haya pale inapoulizwa.
Kama nilivyotambulisha awali maana ya elimu kuwa ni kupata ufunuo kwa jambo usilofahamu, hapa wanafunzi wanaelimishwa mambo mbalimbali na walimu katika utaratibu maalum ambao nchi imejipangia ili kuweza kukamilisha malengo mbalimbali.
Kwa kuwa elimu ni muhimu katika jamii yetu, ubora wa elimu nao ni jambo la msingi katika muktadha wa Nchi yeyote ile. Walimu wanapaswa wapate maslahi bora kuanzia mishahara yao na posho zao ili waweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wao.
Walimu wanapaswa kuwa na nyenzo bora zitakazowawezesha kutoa elimu bora. Mfano wa nyenzo hizi ni kuwa na vifaa vya kisasa vya kufundishia (ICT), maabara bora, maktaba na wanaoelimishwa kuwa na madawati na vitendea kazi. Haya ni baadhi ya mambo muhimu yanayomzunguka mwalimu na mwanafunzi.
Endapo mwalimu atakosa mambo haya ya msingi, basi mwalimu huyu kuna uwezekano mkubwa wa kutotoa elimu bora hivyo taifa kukosa wataalamu watakaoliletea tija taifa letu.
Serikali kwa upande wake inakubali kwamba walimu wanahitaji maslahi bora, wanafunzi pia wanahitaji mazingira bora kiujumla ili waweze kuelimika vizuri, ila tatizo ni uwezo mdogo wa kibajeti. Nijuavyo mimi serikali iliyowekwa madarakani na wananchi inapaswa kutatua kero za wananchi, na si kutoa sababu kwa wananchi ya kutotekeleza ama kutatua kero.
Serikali ni lazima ihitimishe suala hili kwa kutatua kero za walimu kwa kuangalia chanzo na si matokeo, la sivyo kila mwaka kutakuwa na migongano baina yake na jamii katika kada tofauti. Mgomo wa madaktari una kishindo kikubwa kwa kuwa muathirika huenda akafa, lakini kishindo cha mgomo wa walimu ni kibaya zaidi kwa kuwa muathirika hapati elimu bora, hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Mathalani masomo mengi hufundishwa kwa kuwaandaa wanafunzi kinadharia na si vitendo, hii hupelekea wanafunzi kushindwa katika soko la ajira na pia kupungua kwa ubunifu hapa nchini kwetu.
Nahitimisha kwa kupendekeza walimu watekelezewe maslahi yao kwa asilimia mia moja, ili watoto wa wakulima waje wapate fursa katika nchi hii, pia mfumo wa elimu ubadilike uwe wakivitendo zaidi ili tupate wabunifu watakaolivusha taifa hili katika janga la umaskini na kuepuka mambo mengi ya kuiga kutoka kwa wanzetu.
Mkali
No comments:
Post a Comment