Na Maggid Mjengwa,
NAANDIKA haya nikiwa nchini Hispania. Nilipata bahati pia ya kutembelea nchi ya Poland yapata wiki moja iliyopita. Hizi ni nchi mbili ambazo zinafanana katika mambo mawili makubwa; zote mbili zina historia ya kuongozwa kidikteta kabla ya kufikia hatua hii ya kuwa nchi za kisasa na kidemokrasia.
Hispania ilikuwa na utawala wa kidikteta (Dikteta Franco) hadi alipofariki mwaka 1975, ndipo mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yakapamba moto. Poland ilikuwa na udikteta wa chama kimoja ( Ukomunisti) hadi ukuta wa Berlin ulipoangushwa na mageuzi ya kisiasa , kiuchumi na kijamii yalipopamba moto. Na nchi zote hizi mbili ni za Kikatoliki na zina idadi ya watu inayolingana. Zote zina wakazi milioni 40.
Mifumo kandamizi ambayo nchi hizi ilipitia ndiyo iliyosababisha zikawa kwenye matatizo makubwa. Na kubwa zaidi, imani ilikosekana.
Na hakika, tatizo letu kubwa Watanzania kwa sasa ni kukosekana kwa imani miongoni mwetu. Hatuaminiani. Na mfumo uliotufikisha hapa bado hatujaubadili kwa kiwango cha kuridhisha.
Hili ni tatizo la nchi nyingi barani Afrika. Ndiyo, mathalan, Serikali nyingi Afrika hazipendi kuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi kwa vile hutoa nafasi kwa walio kwenye upinzani kuingia madarakani.
Na kwa vile hawana imani nao, kwa maana ya wapinzani, mara na wao watakapoingia madarakani, Serikali hizo huona ni vyema kutokuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi. Hilo la mwisho linawabakishia matumaini ya kuendelea kubaki madarakani. Maana, anayeamua hatima ya uchaguzi si mpiga kura, bali mhesabu kura na mtangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi.
Mfano, katika katiba yetu ijayo, kama itapendekezwa kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi , basi, huo utakuwa ni mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi.
Nahofia Tume Huru ya Uchaguzi itasubiri mpaka tuchinjane kwanza kwa kutuhumiana kuibiana kura kwenye chaguzi. Tatizo ambalo lingeweza kumalizwa kwa kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoaminika na pande zote zinazoshiriki chaguzi. Itakayoaminika na wananchi.
Kuna wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon alitamka; kuwa tatizo kubwa la Serikali nyingi si nakisi ya bajeti bali nakisi ya imani ya Wananchi kwa Serikali hizo. Ndiyo, kupungua kwa imani. Ndiyo, inahusu imani na ni wajibu wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi kuirudisha imani ya wananchi kwa Serikali na chama hicho.
Niliwahi kuandika kuwa nchi yetu iko njiapanda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ‘kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi (wakiwamo viongozi), wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo.
Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi.
Watanzania wengi kwa sasa wana kiu kali ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo.
Na siku zote, nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi bila kuwa na utulivu wa kisiasa. Kuna dalili, huko twendako, hakutakuwa na utulivu wa kisiasa kama tutaicha hali hii ya sasa iendelee kama ilivyo. Hali ya kutoaminiana na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa wa kisiasa.
Na Profesa wa Uchumi, Jeffrey Sachs ana mfano hai wa Poland. Katika kuwashauri kuinuka kiuchumi Wapolandi,
Profesa Sachs aliwaambia; “Political power must be shared”. Kwa tafsiri yangu ni kwamba; kuna umuhimu wa vyama kuwa na utayari wa kugawana madaraka ya uongozi wa kisiasa.
Ndiyo, Fundi Umeme yule Lech Walensa wa chama cha wafanyakazi na aliyeanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kujikomboa kutoka Ukomunisti aliambiwa hivi na Profesa Jeffrey Sachs; “ Chama chako cha Solidarity kiwe radhi kuunda Serikali ya Mseto na Chama Cha Kikomunisti”.
Baada ya uchaguzi ikawa hivyo, kimoja kikatoa Waziri Mkuu na kingine Rais. Kukawepo utulivu wa kisiasa. Poland ikaanza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi. Ndiyo, hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa kisiasa. Katiba Mpya itakayohakikisha, mbali ya mambo ya mengine inatupa Tume Huru Ya Uchaguzi. Nahitimisha.
www.mjengwa.blogspot.com
No comments:
Post a Comment